Asilimia 25 ya vijana Kenya wakumbwa na msongo wa mawazo
UTAFITI mpya umebaini kuwa, asilimia 25 ya vijana wa Kenya walio na umri wa kati ya miaka 11 hadi 25 wanakumbwa na dalili za wastani hadi kali za msongo wa mawazo.
Aidha, takriban asilimia 21.4 ya vijana hao wanaathiriwa na wasiwasi mkubwa huku asilimia 22.6 wakikabiliwa na mawazo ya kujiua, hasa kati ya wale walio na umri wa miaka 15 na zaidi.
Takwimu hizi ni kutokana na utafiti wa Aga Khan Brain and Mind Institute kwa kushirikiana na Shamiri Institute uliowahusisha vijana 2,842 kutoka shule 42 za upili kote nchini.
Kwa mujibu wa Profesa Zul Merali, mkurugenzi mwanzilishi wa Aga Khan Brain and Mind Institute, kiwewe utotoni kama vile dhuluma, umasikini, kutelekezwa na unyanyasaji una madhara ya kudumu kwenye tabia, fikra na hisia za mtu.
“ Tunahitaji mikakati ya kitaifa ya kuvunja mzunguko huu wa mateso,” alisema.
Utafiti huo ulionyesha kuwa mmoja kati ya vijana watano (asilimia 20) amekumbana na visa vinne au zaidi vya matukio mabaya wakiwa watoto, kama unyanyasaji wa kimwili au kingono, ukosefu wa mahitaji ya msingi, au kushuhudia vurugu za nyumbani.
Watafiti walibaini kuwa vijana walio na mzazi mmoja waliathirika zaidi kwa asilimia 18 ikilinganishwa na wale walio na wazazi wote wawili.
Wale walio na matatizo ya kitaaluma pia walionekana kuwa na uwezekano wa asilimia 15 zaidi wa kuwa na matatizo ya kihisia au kiafya ya akili.
Kwa mujibu wa Tom Osborn, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shamiri Institute vijana wanabeba mizigo mikubwa ya kihisia.
“Ukatili wa kijinsia, unyanyapaa na dhuluma vinaathiri sana afya yao ya akili. Tuna jukumu la kuhakikisha shule zinakuwa mahali pa uponyaji,” alisema.
Utafiti huo unaonya kuwa kutoshughulikia matatizo ya akili kunaweza kusababisha matumizi ya dawa za kulevya, kudorora kwa tabia na kupunguza uwezo wa vijana kuchangia uchumi wa taifa.