Habari

Asilimia 92 ya maji ya Ziwa Victoria ni kinyesi na sumu!

February 16th, 2020 2 min read

Na PAUL WAFULA

SAMAKI wanaovuliwa kutoka Ziwa Victoria wana madini ambayo ni sumu kwa mwili wa mwanadamu, uchunguzi wa Taifa Leo umegundua.

Sampuli za maji zilizopimwa zilionyesha kuwa asilimia 92 ya Ziwa Victoria imechafuka hasa kutokana na kinyesi cha binadamu na madini yenye sumu.

Iligunduliwa pia kuwa mito ipatayo 10 inayomimina maji ziwani humo pia inamwaga virusi vinavyoweza kusababisha magonjwa.

SOMA PIA:

Maji ya chupa yamejaa chembechembe za kinyesi – Ripoti

Sumu mitoni yatishia maisha ya mamilioni ya Wakenya

Hofu Ziwa Victoria likinyakuliwa na wafanyabiashara

TAHARIRI: Serikali ishughulikie ripoti ya uchafuzi

Samaki wote waliochunguzwa walipatikana kuwa na aina mbalimbali za madini ambayo ni pamoja na risasi, cadmium, chromium, zinc, iron, copper na manganese.

Hata hivyo, baadhi ya madini hayo ni ya viwango vinavyokubalika kiafya.

Lakini samaki waliovuliwa katika ufuo wa Marenga nchini Kenya, Masese na Gabba nchini Uganda pamoja na wa kutoka China walipatikana kuwa na viwango hatari vya risasi.

Madini ya risasi husababisha saratani, uhaba wa damu na nguvu mwilini pamoja na madhara ya figo na ubongo.

Samaki katika maeneo hayo pia walipatikana kuwa na kiasi cha juu cha zinc na mercury ambayo ina madhara kwa ubongo, roho, figo, mapafu na kinga ya mwili pamoja na tumbo.

Uchunguzi huo pia ulionyesha kuwepo kwa mabaki ya dawa 25 za kuua wadudu kwenye maji ya kunywa.

Kwenye mito inayomimina maji Ziwa Victoria, Mto Awach ulipatikana kuwa na kiasi kikubwa zaidi cha madini hatari ukifuatwa na Mto Kisat na Mto Migori.

Kwenye ziwa, maji katika eneo la Homabay yalipatikana kuwa chafu zaidi ikifuatwa na yale ya Kendu Bay, Mto Sondu na ufuo wa Kisumu. Hii inatokana zaidi na umwagaji wa taka.

Kulingana na uchunguzi huo wa kina ulioshirikisha wanasayansi, Ziwa Victoria, ambalo ndilo kubwa zaidi Afrika lina uchafu na sumu ambazo zimesababisha kuangamia kwa aina kadhaa za samaki.

Uchafuzi huo ni mwingi zaidi karibu na nchi kavu kuliko kati mwa ziwa.

Kati ya dawa za kuua wadudu zilizopatikana ni DDT ambayo imepigwa marufuku nchi zingine kwa kusababisha kansa, endosulfan inayodhuru watoto wachanga na mirex ambayo pia husababisha saratani.