Habari

Askofu Muheria atumia Jumatano ya Majivu kusuta viongozi waongo, walio na majivuno

Na JOSIAH MUGO March 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ASKOFU Mkuu wa Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria amewataka viongozi kutumikia kwa unyenyekevu na kusema ukweli wanapohudumia umma.

Akizungumza wakati wa ibada ya Jumatano ya Majivu mjini Nyeri, Askofu huyo alikumbusha viongozi kwamba licha ya madaraka na mamlaka yao, haimaanishi kwamba hawana mapungufu na dhambi.

“Wengi wetu tunajitangaza kuwa watakatifu, lakini ndani ya mioyo yetu tunajua kuwa tumejaa mapungufu na makosa,” alisema.

Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria wakati wa Ibada ya Jumatano ya Majivu, Machi 5, 2025 ambapo alitaka viongozi wahudumu kwa ukweli na unyenyekevu. Picha|Josiah Mugo

Licha ya ugumu, lazima tuendelee kuwa na matumaini

Alisisitiza kuwa uongozi wa kweli unatokana na kujitambua, huruma, na huduma kwa wengine, hasa masikini na waliosahaulika.

Askofu alisisitiza kwamba viongozi lazima waongee ukweli kwa watu wanaowategemea, wakitoa mwongozo kwa uaminifu.

“Jukumu lenu si kuongoza tu bali pia kusema ukweli, hata pale ambapo ni vigumu,” alishauri, akisisitiza uwajibikaji wa kimaadili unaotarajiwa kutoka kwa viongozi.

Mbali na wito huo wa unyenyekevu, Muheria alitoa ujumbe wa matumaini kwa wananchi wa Kenya, hasa katika nyakati hizi zilizo na changamoto tele.

Alikubali kuwa masaibu ni mengi, ila akawahimiza waendelee kuwa na matumaini na kuendelea kusali.

“Licha ya ugumu, lazima tuendelee kuwa na matumaini,” alisema.