Habari

Askofu Ole Sapit awataka wanasiasa wapunguze joto la 'kampeni za 2022'

January 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Kanisa la Anglikana Nchini (ACK) Jackson Ole Sapit amewataka wanasiasa kupunguza joto la kisiasa mwaka huu wa 2020 na badala yake waangazie mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazowasibu Wakenya.

Akiongea na wanahabari Jumatano baada ya kuongoza Ibada ya kukaribisha Mpaka Mpya katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi, Ole Sapit alitaja matatizo kama ukosefu wa ajira, ufisadi, ukabila, kupanda kwa gharama ya maisha kama ambayo viongozi wa kisiasa wanapaswa kushughulikia wala sio kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

“Najua itakuwa vigumu kwa viongozi wetu kukomesha siasa haswa za uchaguzi mkuu ujao, lakini nawahimiza kwamba wananchi hawataweza kuwapigia kura ikiwa matatizo yanayowazonga wakati hayatatuliwa. Kwa hivyo, ni wajibu wao kuhakikisha kuwa vijana wanapata ajira na gharama ya maisha inashuka,” akasema.

 

Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit akiongea na wanahabari Jumatano, Januari 1, 2020, baada ya kuongoza ibada ya kufungua Mwaka katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi. Amewahimiza wanasiasa kupunguza siasa na badala yake washughulikie changamoto zinazowasibu Wakenya. Picha/ Charles Wasonga

Vilevile, Dkt Ole Sapit amewaonya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) bali waitumie kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowasibu Wakenya.

“Ripoti ya BBI haifai kutumiwa kama jukwaa la kubuni miungano ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022. Kama Kanisa tunahimiza kuwa ripoti hii itumiwe kuanzisha mdahalo wa kitaifa kuhusu yale yanayotutatiza kama taifa na namna ya kuyatatua. Tutumie BBI kupalilia umoja wa kitaifa,” akasema.

Ole Sapit ametoa changamoto kwa viongozi wa kisiasa kutumia muda wao mwingi mwaka huu kutekeleza ahadi walizowapa wapiga kura.

“Rais na naibu wake wawe mstari wa mbele kuongoza mipango ya kutekeleza manifesto yao na ahadi zote walizotoa kwa Wakenya mwaka 2017. Na wabunge nao watumie pesa za CDF kwa miradi yenye manufaa kwa wananchi,” akasema.

Kiongozi huyo wa ACK pia amewataka viongozi wawe kielelezo bora kwa vijana kwa kutembea katika mwangaza na kuepukana na maovu na vitendo vinginevyo vinavyokwenda kinyume na sheria.

“Viongozi wakitembea katika mwangaza watafanya maamuzi mazuri na vitendo vyao vitakuwa vya kupigiwa mfano. Sisi kama viongozi wa kidini na wenzetu wa kisiasa tunastahili kufanya mambo ambayo yatanufaisha jamii bali sio kuigawa,” akasema.