Habari

Atwoli aanikwa na mkewe jinsi ameshindwa na majukumu ya nyumbani

August 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

REKODI ya mawasiliano ya simu kati ya kiongozi wa Muungano wa Vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli na mkewe ‘Rose’ imeibua hisia kote nchini, katika mazungumzo yanayoashiria kuwa kiongozi huyo ameshindwa kutelekeza majukumu ya familia yake, japo mbele ya umma akivaa sura ya mwanaume mwenye msingi.

Mazungumzo hayo ya dakika saba na zaidi ya sekunde 40 yanahusisha Bw Atwoli na Bi Rose wakishiriki katika mazungumzo yaliyotawaliwa na kugombana na kubishana, huku mke huyo akidai mumewe Atwoli alimuacha.

Kulingana na mazungumzo hayo ambayo uwezekano kuwa yalifanyika kabla ya uchaguzi uliopita uko juu, kiini cha mzozo baina yao ni kuwa Bi Rose alitaka kugombea kiti cha siasa, japo Bw Atwoli naye alikuwa akipinga.

“Mimi nilikuuliza, unagombea katika uchaguzi ujao?” Bw Atwoli anaanza baada ya kumzomea mkewe huyo kuwa alikuwa amemkatia simu.

Baada ya mwanamke kukiri kuwa angependa kuwania, Bw Atwoli anamtishia kuwa atamtaliki.

“Sikiza Rose, mimi ndio najua wewe akuna kitu unajua, ile kitu ninaona wewe huwezi kuona,” anasema Atwoli.

Bi Rose naye anapasuka kuwa Atwoli amemnyima haki zake za kindoa na kukataa kumtimizia mahitaji ya kimsingi kwa miezi kumi, hadi wakati walipokuwa wakizungumza.

 

‘Usiwe dikteta’

“Kutoka mwaka jana Disemba hujawahikurudi hapa, sasa ni Oktoba tutawahizungumza lini,” anauliza Bi Rose, akiongeza “Usiwe dikteta, pia mimi ni binadamu.”

“Francis wacha nikwambie, watoto wangu umekataa kunisaidia kusomesha, mimi niko na majukumu ya kuwatunza wazazi wangu. Ninakuelewa kuliko unavyodhani, tangu uliponioa, hujawahi kuwa na malengo mema name wala wanangu,” anasema Bi Rose.

Lakini Bw Atwoli anamlaumu mkewe kwa kumchafulia penzi na wanaume masikini, akisema ndiyo sababu aliamua kumuacha.

“Baadhi ya hawa wanaume unaoshiriki nao ni wale masikini zaidi kote Afrika,” Bw Atwoli anadai.

Lakini mkewe anakana, akimwambia kuwa japo ni kweli kuwa kiongozi huyo ni bilionea, yeye kama mke wake anakosa hadi shilingi kumi na kuishia kuuza mali ili kujikimu.

“Wewe ni tajiri lakini utajiri wako unakufaidi wewe peke yako, mimi hukosa hata shilingi kumi kwa mfuko hadi nauza shamba na mali nyingine. Wewe ni kiongozi wa kitaifa lakini huongozi kutoka nyumbani, sasa una mtoto ambaye hajakuona kutoka mwaka uliopita, hii inaadhir mtoto huyu,” anasema Bi Rose.