Baba na wanawe wawili kunyongwa kwa kumuua mvulana mchungaji
BRIAN OCHARO Na PETER MBURU
BABA na wanawe wawili wa kiume Jumanne walihukumiwa kifo na mahakama moja ya Kwale, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mvulana wa kuchunga mifugo miaka mitatu iliyopita katika eneo la Chidi, kaunti ya Kwale.
Alipokuwa akiwahukumu watatu hao, Jaji Asenath Ongeri alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulidhihirisha kuwa Bw Mudata Mwamumbo Ndolo na wanawe Mwachodo Mudata na Mwamumbo Mudata (kwa jina la utani Madvi) walimuua kijana huyo ambaye alikuwa wa chini ya miaka 18 kwa kumvunja shingo, kisha wakatupa mwili wake majini.
“Baada ya kukagua ushahidi uliotolewa, napata kuwa washukiwa walihusika kwa pamoja kumuua Silipano Ndooki,” akasema Jaji huyo.
Alisema kuwa mahakama ilibaini Bw Ndolo alivunja shingo ya marehemu na kusaidiwa na Bw Madvi ambaye alimshika marehemu, ilhali Bw Mudata aliubeba mwili hadi kwenye maji na kuwekelea jiwe juu yake.
Jaji huyo alisema kuwa watatu hao walikuwa wakilipiza kisasi baada ya mifugo 800 wa babake marehemu kuvamia shamba lao na kuharibu mimea.
Korti ilielezwa kuwa Bw Ndolo alikataa kupokea ridhaa ya Sh7,000 kutoka kwa familia ya marehemu baada ya mimea kuharibiwa na kudai Sh60,000. Korti ilisikia kuwa alitishia kulipiza kisasi ikiwa pesa hizo hazingelipwa.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Ongeri alisema washukiwa walimuua mvulana ambaye hakuwa na hatia na hivyo hawakufaa kuhurumiwa.
“Ninapata kuwa washukiwa walitekeleza kitendo cha unyama hivyo kwa mvulana ambaye hakuwa na hatia na ambaye alikuwa tu akichunga mifugo na hivyo hawafai kuhurumiwa, ijapokuwa wana familia zinazowategemea. Maisha yamepotezwa na familia ya marehemu imempoteza milele,” akasema.