Babu Owino akamatwa baada ya tukio la ufyatuaji risasi
VINCENT ACHUKA na HARRY MISIKO
MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amejikuta tena pabaya mara hii akidaiwa kujihusisha katika ufyatulianaji risasi ambapo inadaiwa alimjeruhi mcheza muziki yaani DJ wa kilabu maarufu Kilimani, Nairobi.
Maafisa wa polisi wamemkamata mwanasiasa huyo wa ODM Ijumaa asubuhi muda mchache baada ya tukio la saa kumi za asubuhi katika B Club katika barabara ya Galana jijini Nairobi.
Ripoti ya polisi ambayo Taifa Leo imeona inasema mbunge huyo alichomoa bastola na kumlenga na kumfyatulia risasi DJ kwa jina Felix Orinda, hii ikiwa ni baada ya kutokea majibizono makali.
“Alichomoa bastola akamfyatulia DJ shingoni. Majeruhi amewahiwa katika Nairobi Hospital akiwa katika hali isiyo nzuri hii ikiwa ni baada ya usimamizi wa kilabu kuingilia kati,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Wapelelezi wamesema wangali wanafanya uchunguzi na kuitafuta silaha iliyotumika.
“Maafisa wapo eneo la tukio wakitafuta maganda ya risasi iliyotumika,” inasema ripoti hiyo.
Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) imethibitisha kukamatwa kwa Owino.
“Mbunge huyo anazuiliwa ili akahojiwe zaidi,” DCI imesema kwenye chapisho katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.
Owino amesafirishwa kwa gari hadi kituo cha polisi cha Kilimani ambako alikuwa akizuiliwa hadi wakati tunachapisha habari hii.