BAJETI: Ujenzi wa reli, elimu zapewa kipaumbele
Na CAROLYNE AGOSA
UJENZI wa barabara na reli mpya ya SGR, uimarishaji elimu na uhifadhi mazingira zimepewa kipaumbele katika bajeti ya serikali ya mwaka 2019.
Katika Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 utakaoanza Julai 1, sekta ya usalama na hususan idara za polisi na jeshi pia zitanufaika na ufadhili mkubwa.
Wasiojiweza katika jamii, vijana na wanawake pia wamepewa mgao mkubwa kwenye makadirio hayo yanayoonyesha jinsi serikali inapanga kutumia fedha katika miezi 12 ijayo. Bajeti hiyo ya Sh Sh2.53 trilioni iliwasilishwa Alhamisi katika Bunge la Kitaifa na Kiongozi wa Wengi, Bw Aden Duale.
Inalenga hususan kufadhili ajenda nne kuu za Rais Uhuru Kenyatta kwa kitita cha Sh460 bilioni.
Ajenda hizo ni: chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi, huduma bora za afya kwa kila Mkenya, kujenga takriban nyumba 500,000 za bei nafuu ifikapo 2022, na kuimarisha uzalishaji bidhaa nchini.
Serikali imetenga Sh6.76 bilioni kwa miradi mbalimbali ya kunyunyiza maji mashamba kwa lengo la kuzalisha magunia milioni 2.76 ya mahindi, viazi na mchele. Vilevile, hifadhi ya kitaifa ya chakula cha dharura itapokea Sh1.42 bilioni huku mpango wa kuimarisha uzalishaji nafaka ukipokea Sh1.89 bilioni.
Wakulima nchini watapata afueni baada ya mbolea iliyopunguzwa bei kutengewa Sh4.3 bilioni. Vilevile, serikali imetenga Sh300 milioni kukabiliana na mdudu sugu wa viwavijeshi. Kupunguza hasara zinazotokea baada ya wakulima kuvuna mazao yao serikali imetenga Sh300 milioni kwa bima ya mimea.
Sekta ya elimu imetengewa Sh194.9 bilioni. Serikali ya Jubilee imeazimia kutimiza ahadi ya kutoa elimu ya shule za upili bila malipo kwa kutenga Sh59.4 bilioni kufadhili mpango huo. Elimu ya msingi bila malipo imetengewa Sh13.4 bilioni.
Serikali pia inanuia kutimiza ahadi ya kuondoa ada ya mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa shule za umma ; imetenga Sh4 bilioni kugharamia ada hizo.
Serikali itatumia Sh6 bilioni kuajiri walimu wapya. Vilevile, Sh2.3 bilioni zitatumika kwa lishe ya wanafunzi.
Vyuo vikuu ndivyo vitanufaika zaidi katika bajeti ya mwaka ujao ya elimu baada ya kutengewa Sh90.5 bilioni.
HELB yapungua
Hata hivyo, ufadhili kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) umepungua hadi Sh9.6 bilioni kutoka Sh10.1 ilizopewa mwaka wa sasa wa fedha 2017/2018.
Upunguzaji huo umetokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu vya umma– kutoka wanafunzi 564,507 mwaka jana hadi 520,893 mwaka huu.
Taasisi za mafunzo ya kiufundi zitapokea Sh9.7 bilioni katika juhudi za kuimarisha ujuzi wa kiufundi nchini.
Serikali imezingatia athari za mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini kwani imetenga Sh60.4 bilioni za kukabiliana na mafuriko, kuhifadhi maji na kulinda mazingira.
Ujenzi wa mabomba ya maji na maji taka utapata sehemu kubwa ya fedha hizo – Sh31.2 bilioni, huku miradi ya kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji ikitengewa Sh10.8 bilioni.
Masikini, wakongwe, walemavu, mayatima, wanawake na vijana watanufaika na hazina mbalimbali ambazo zimetengewa jumla ya Sh53.9 bilioni. Hata hivyo, kuna hatari ya fedha za wakongwe kukauka kabla mwaka wa fedha kukamilika.
Serikali imewatengea Sh5.1 bilioni pekee licha ya hazina hiyo kuhitaji Sh15.6 bilioni kuwafaa wakongwe hao 523,129 waliokuwa wamesajiliwa kufikia Machi.
Afya
Katika sekta ya afya serikali ya Jubilee imetenga Sh44.6 bilioni zitakazofadhili masuala mbalimbali ikiwemo Mpango wa Kukodisha Vifaa vya Matibabu (MES) kwa hospitali kuu za kaunti; na mpango wa huduma za afya bila malipo kwa akina mama na watoto ambao awali uligharamia tu huduma za kujifungua.
Sehemu kubwa ya fedha hizo pia itapewa hospitali kuu za rufaa nchini: Kenyatta (Sh9.4 bilioni) na Moi mjini Eldoret (Sh6.2 bilioni). Taasisi za mafunzo na utafiti wa matibabu zitapokea jumla ya Sh5.3 bilioni huku wahudumu wa afya wanagenzi wakitengewa Sh2.9 bilioni.
Mradi wa kusambaza umeme nchini, kuweka taa barabarani, kuimarisha usambazaji umeme katika maeneo bunge, kupunguza ada ya kuwekewa umeme nyumbani, kukuza kawi inayotokana na mvuke, ugunduzi na usambazaji wa mafuta na gesi ni baadhi ya miradi iliyotengewa Sh45.3 bilioni katika sekta ya kawi.
Wizara ya Fedha imetenga Sh45.3 bilioni kwa ajenda ya Rais Kenyatta ya kujenga nyumba 500,000 za bei nafuu kufikia 2022, kuimarisha mitaa ya mabanda, kujenga nyumba za polisi na askari wa magereza, kuimarisha utoaji huduma katika jiji la Nairobi na viunga vyake, na ustawi wa miji nchini.