HabariSiasa

BBI inavyowatakasa washukiwa

March 5th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MPANGO wa Maridhiano (BBI) umeibuka kuwa kidimbwi cha kuwatakasa viongozi wanaokabiliwa na mashtaka ya ufisadi na uhalifu.

Hii ni baada ya vinara wakuu wa BBI wakiongozwa na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kuwakumbatia wanasiasa walio na kesi kortini baada ya kutangaza kuwa wanaunga mkono BBI.

Wadadisi wanasema viongozi walio na kesi mahakamani wamegundua kuna fursa ya sifa zao kuoshwa machoni pa raia ndiposa wanaimba wimbo wa BBI.

“Raila Odinga sasa ndiye sabuni ya kuosha wahalifu. Ikiwa wewe ni mwizi, usijali, msalimie tu Raila na utaoshwa makosa yako,” mwanaharakati Bonface Mwangi akasema.

Kiongozi wa chama cha Third Way Alliance Ekuru Aukot alikubaliana na kauli hiyo akisema BBI imebadilika kuwa pango la washukiwa wa uhalifu.

“BBI inatakasa uhalifu. Pia imezaa makuhani wakuu wa kuosha sifa za washukiwa kwa kisingizio cha kuunganisha Wakenya. Imekuwa maficho ya washukiwa wa uhalifu,” alisema Bw Aukot.

Kulingana na mwanaharakati Ndung’u Wainaina, washukiwa wa ufisadi na uhalifu wanahitaji tu kujiunga na kampeni ya BBI ili sifa zao mbaya ziweze kutakaswa.

Wakili Ahmednasir Abdullahi naye alizua hoja kuwa siku hizi hata kortini mtu anaweza kuondolewa makosa iwapo wakili atamwambia hakimu kuwa mteja wake anaunga mkono BBI.

“Utetezi wako kama wakili kuwa mteja wako anaunga mkono BBI una nguvu kiasi cha kuwezesha mshtakiwa kuachiliwa mara moja, kuondolewa mashtaka, kusimamishwa kwa uchunguzi kisha mshukiwa huyo anapewa kiti cha mbele na nafasi ya kuhutubu kwenye mikutano ya BBI,” akasema kwenye Twitter

Ingawa bado hawajapatikana na hatia, kabla ya BBI washukiwa hao walikuwa wametengwa na hawakuwa wakionekana wakitangamana na viongozi wakuu.

Hata magavana ambao walikuwa wakichunguzwa kwa ufisadi wamejiunga na gari moshi la BBI licha ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuorodhesha vita dhidi ya ufisadi kuwa moja ya malengo makuu ya mchakato huo.

Gavana Okoth Obado wa Migori ni miongoni mwa viongozi ambao wamekumbatiwa licha ya kuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama Kuu.

Baada ya Obado kushtakiwa kwa mauaji ya Sharon Otieno, alionekana kuegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto huku viongozi wa ODM akiwemo Bw Odinga wakijitenga naye.

Lakini tangu alipoamua kuunga mkono BBI, Bw Obado amekumbatiwa na wakuu wa ODM na amekuwa akipewa nafasi za kuhutubu katika mikutano ya mchakato huo.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alipokamatwa na kushtakiwa kwa jaribio la kumuua DJ Evolve, chama cha ODM kilijitenga na masaibu yake kikisema alikuwa ametekeleza uhalifu.

Wenzake wa ODM hawakutaka kuhusishwa na Bw Owino wakati huo hadi alipoachiliwa kwa dhamana na kujiunga na BBI ambapo sasa amekuwa akitambuliwa kwa taadhima kuu.

“ODM ni chama kilicho chini ya sheria za nchi. Kwa wakati huu, wasiwasi wetu ni kuhusu mwathiriwa wa tukio hili la kuhuzunisha,” Katibu Mkuu Edwin Sifuna alinukuliwa wakati kisa hicho kilipotendeka.

Lakini sasa ambapo Bw Owino anaunga BBI, hakuna anayezungumzia hali ya DJ Evolve ambaye angali hospitalini.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko anakabiliwa na kesi ya wizi wa mamilioni ya pesa za kaunti na alipokuwa akikamatwa na kushtakiwa alitengwa na wanasiasa wenzake wa Jubilee.

Ingawa hajahudhuria mikutano ya BBI, ametangaza anaiunga mkono kwa dhati.

Majuzi Rais Uhuru Kenyatta aliwaomba madiwani wa Nairobi kusitisha juhudi zao za kumwondoa madarakani.

Gavana Moses Kasaine wa Samburu naye ana kesi ya ufisadi kortini lakini sasa anashiriki jukwaa moja na Bw Odinga.

Kinaya ni kwamba katika mikutano ya BBI, Bw Odinga amekuwa akikashifu ufisadi huku baadhi ya wanaokabiliwa na mashtaka wakiwa wameketi katika jukwaa moja naye.