HabariSiasa

BBI: Jiandae kwa kivumbi, Kamket amwambia Ruto

December 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FLORAH KOECH

MBUNGE wa Tiaty, Bw William Kamket, amemtaka Naibu Rais William Ruto na wandani wake kujitayarisha kwa “wimbi la kisiasa” litakaloletwa na ripoti ya Jopokazi la BBI.

Bw Kamket alisema kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kura ya maamuzi, kinyume na kupelekwa Bungeni kama inavyopendekezwa na washirika wa Dkt Ruto.

Akizungumza mnamo Jumatatu katika eneo la Chesotim, wadi ya Tirioko, Bw Kamket alisema kuwa ingawa baadhi ya sehemu za ripoti hiyo zinahitaji kutathminiwa upya, mapendekezo mengi yaliyopo ni mazuri.

“Kuna baadhi ya sehemu za ripoti hiyo zinahitaji kubadilishwa, likiwemo pendekezo kuhusu Waziri Mkuu, kwani anapaswa kupewa mamlaka zaidi. Baada ya mabadiliko hayo, ripoti itakuwa tayari kuwasilishwa kwa wananchi,” akasema Bw Kamket.

Aliwakosoa baadhi ya wabunge wa mrengo wa ‘Tanga Tanga’ ambao wamekuwa wakipinga maandalizi ya kura ya maamuzi.

Alishangaa sababu ambapo baadhi ya wabunge hao wamekuwa wakiipinga kura hiyo, licha ya kudai kuwa wanaunga mkono ripoti hiyo.

“Tunashangaa sababu ya baadhi ya washirika wa Dkt Ruto kuwa na wasiwasi kuhusu kuandaliwa kwa kura ya maamuzi. Nimewaona wabunge wenzangu kutoka maeneo ya Kati na Bonde la Ufa wakiliogopa zoezi hilo, ilhali wamekuwa wakidai kuwa wana uungwaji mkono mkubwa katika maeneo yao,” akasema.

“Katiba si stakabadhi ya kuchezea katika Bunge la Kitaifa. Ni lazima iamuliwe na Wakenya. Ni wao watakaoamua yale wanayotaka kupitia kura ya maamuzi na si kupitia Bunge, kwani wabunge wanaongozwa na maslahi yao binafsi,” akaeleza.

Alimlaumu Dkt Ruto kwa kuwatumia baadhi ya wabunge kutoka maeneo hayo mawili kuendeleza msimamo wake kuhusu ripoti hiyo.

“Tunashangazwa na hatua ya Dkt Ruto kuendeleza mikutano ya kisiasa kwa kuwatumia wabunge hao. Ningetaka kumweleza kuwa idadi kubwa ya wanasiasa hao hawatachaguliwa tena ifikapo 2022,” alisema Bw Kamket kwenye ujumbe uliomlenga Dkt Ruto.

Aliongeza, “Ikiwa unategemea hao, basi unapaswa kujitayarisha kwa wakati mgumu kisiasa.”

Kiongozi huyo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Seneta Gideon Moi wa Baringo, pia alimkashifu vikali Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen kwa kudai kuwa bado hajayaona mawimbi ya kisiasa ya ripoti hiyo kama ilivyodaiwa na baadhi ya wanasiasa.