BBI kuwapokonya wabunge na madiwani marupurupu ya mamilioni
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE na maseneta watapoteza takriban Sh67 milioni ambazo wao hupokea kama marupurupu kila mwezi ikiwa pendekezo la Mpango wa Maridhiano (BBI) kuhusu marupurupu ya watumishi wa umma litapitishwa.
Ripoti hiyo ambayo ilipokezwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wiki jana, inafutilia mbali marupurupu ya vikao kwa watumishi wa umma ili kuokoa mabilioni ya fedha za umma.
Kwa mujibu wa kipengele cha 260 cha pendekezo la marekebisho ya Katiba, wabunge, maseneta na madiwani wameorodheshwa kama maafisa wakuu wa serikali (state officers).
Wakati huu, jumla ya wabunge na maseneta 416 hupokea Sh5,000 kila mmoja kama marupurupu ya kuhudhuria vikao rasmi na vile vya kamati za bunge la kitaifa na lile la seneti.
Kulingana na mwongozo uliotolewa na Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) mnamo 2017 mbunge anaruhusiwa kuhudhuria vikao vya mijadala visivyozidi 16 kila mwezi. Vile vile, wako huru kuhudhuria angalau vikao 16 vya kamati kwa mwezi mmoja.
Hii ina maana kuwa mbunge au seneta anaweza kutia kibindoni Sh160,000 kwa mwezi kama marupurupu ya vikao pekee, kando na mishahara yao.
Nao madiwani hupokea marupurupu ya Sh3,000 za kuhudhuria vikao vya kamati na Sh5,000 kwa kuhudhuria vikao rasmi vya mijadala.
Kulingana na mwongozo wa SRC, madiwani hawaruhusiwi kupokea zaidi ya Sh124,000 kila mwezi kama marupurupu ya vikao.
Hii ina maana kuwa madiwani wote 2,222 ambapo 1,450 wanawakilisha wadi na wengine 772 ni madiwani maalum, hutia kibindoni Sh124 milioni kila mmoja kila mwezi kama marupurupu ya vikao ikiwa wote watahudhuria vikao hivyo.
SRC ilifutilia mbalimbali marupurupu ya vikao kwa watumishi wa umma mnamo 2017 lakini wabunge wakaelekea kortini kupinga hatua hiyo. Mahakama ilibatilisha hatua hiyo ya SRC.
Wengine walioathirika na pendekezo hilo ni maafisa wa umma ambao wameteuliwa kuketi katika bodi za wasimamizi wa mashirika ya serikali.
Kando na mishahara yao ya kila mwezi, maafisa hao hupokea marupurupu wanapohudhuria na kushiriki katika mikutano ya bodi za mashirika hayo.
Ripoti hiyo ya BBI pia inapendekeza kuwa kamati maalum ibuniwe itakayofanyakazi na SRC kusawazisha marupurupu na mishahara ya watumishi wote wa umma.