HabariSiasa

BBI: Rais kuteua Waziri Mkuu, kuendelea kuchaguliwa na raia

November 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER NGARE

WAKENYA wataendelea kuchagua Rais moja kwa moja kama ilivyo kwenye Katiba ya sasa iwapo mapendekezo ya Jopo la Maridhiano (BBI) yataidhinishwa.

Kulingana na mapendekezo ya jopo hilo lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kwa uchache Rais atachaguliwa kwa asilimia 50 ya kura zilizopigwa na nyongeza ya moja.

Kinyume na ilivyokuwa ikidhaniwa kabla ya ripoti hiyo kutolewa jana, Rais ataendelea kuwa kiongozi wa serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Pia atakuwa mwenyekiti wa vikao vya Baraza la Mawaziri ambalo litajumuisha Naibu Rais, Waziri Mkuu na mawaziri watakaoteuliwa ndani na nje ya Bunge.

Kulingana na mapendekezo ya BBI, kutakuwa na Waziri Mkuu ambaye atakuwa kinara wa mawaziri ambao ndio watakuwa watekelezaji wa sera za Serikali Kuu.

BBI inapendekeza mawaziri wawe wakiwajibika kwa Bunge kwa kile inachosema ni kuwajibikia wananchi kwani wabunge ndio wawakilishi wa raia.

Jopo hilo pia limedumisha Rais awe akihudumu kwa kipindi cha awamu mbili kama ilivyo kwa sasa.

Pia limepedekeza wadhifa wa Naibu Rais uendelee kuwepo chini ya Katiba ya sasa ilivyo.

Kulingana na ripoti hiyo, Kenya itakuwa na Waziri Mkuu ambaye atateuliwa na Rais kutoka chama chenye idadi kubwa zaidi ya wabunge, ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) inapendekeza.

Iwapo hakutakuwa na chama chochote chenye idadi kubwa ya wabuge kuliko vingine.

Rais atamteua aliye na uungwaji mkono kutoka kwa idadi kubwa ya wabunge kwa jumla.

Baada ya kuteuliwa na Rais, Waziri Mkuu ataidhinishwa na wabunge kwa kupigiwa kura na wengi.

Iwapo aliyeteuliwa atakataliwa na Bunge, Rais atamteua mwingine hadi kupatikane Waziri Mkuu atakayekubalika.

Mamlaka hayo ya Rais kuteua Waziri Mkuu yanamaanisha kuwa pia atakuwa na uwezo wa kumfuta kazi.

Waziri Mkuu pia anaweza kupoteza wadhifa huo kwa kura ya kutokuwa na imani naye Bungeni.

Ripoti hiyo ya BBI inapendekeza Waziri Mkuu ndiye atakayekuwa na madaraka ya kusimamia shughuli za utekelezaji wa sera za Serikali Kuu kupitia kwa Mawaziri na pia atakuwa ndiye Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.

“Waziri Mkuu pia ataongoza kamati ndogo za Baraza la Mawaziri kama atakavyoelekezwa na Rais na atatekeleza maagizo yote ambayo Rais ataagiza yatekelezwe,” yasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa Waziri Mkuu hatalipwa pesa zozote zaidi ya mshahara wake kama mbunge.

Katika juhudi za kuzuia kuingizwa kwa siasa katika uteuzi wa makatibu wa wizara, BBI inapendekeza walioteuliwa katika wadhifa huo wasiwe wakipigwa msasa na Bunge kama ilivyo kwa wakati huu.

Jopo hilo pia limependekeza kuwa mawaziri watakuwa wakiteuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

Mawaziri hao, inasema ripoti hiyo, watakuwa wakiteuliwa kutoka miongoni mwa wabunge na pia wanaweza kuwa wataalamu ambao si wabunge.

“Mawaziri ambao watateuliwa kutoka nje ya Bunge watachukua vyeo vya ubunge baada ya kuidhinishwa na Bunge,” inapendekeza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inapendekeza pia kuwe na manaibu wa mawaziri ambao pia watakuwa ni wabunge.Mawaziri na manaibu wao, inasema BBI, hawatalipwa mshahara zaidi juu ya ule wanaolipwa kama wabunge