BBI: Ruto atapatapa
Na BENSON MATHEKA
NAIBU Rais William Ruto anaonekana kuchanganyikiwa kuhusu hatua thabiti anayofaa kuchukua kuhusu mswada wa kubadilisha katiba ambao amekuwa akipinga.
Dkt Ruto alikuwa akiongoza vuguvugu lake la walala-hoi maarufu kama mahasla, waliokuwa wakimuunga mkono kwa kupinga mchakato huo akidai alikuwa akitetea maslahi yao.
Katika siku mbili zilizopita, Dkt Ruto ameashiria kuwa huenda akaunga mswada huo ingawa baadhi ya wandani wake wameahidi kuupinga.
Jumamosi, alisema hana nia ya kuzua upinzani katika juhudi za kupinga mswada huo licha ya baadhi ya wandani wake kutangaza wangeupinga.
Hakuhudhuria uzinduzi wa kukusanya saini za kuunga mswada huo mnamo Jumatano katika Ukumbi wa KICC hafla iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Licha ya kukosa kuhudhuria, baadhi ya masuala aliyolalamikia wakati ripoti hiyo ilipozinduliwa katika ukumbi wa Bomas, yalitekelezwa, hatua ambayo wachanganuzi wanasema hakutarajia.
Hata hivyo, Dkt Ruto, Jumamosi aliwakemea wanaotaka apinge mswada huo akisema wanataka kugawanya Wakenya.
Duru zinasema kushughulikiwa kwa masuala hayo kumemuacha katika hali ya kuchanganyikiwa kwa sababu wandani na wafuasi wake walikuwa tayari kumuunga kupinga mswada huo.
Baadhi ya wachanganuzi wanasema kwamba ameng’amua ingekuwa mlima kwake kufadhili kampeni ya kupinga mswada huo miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu ambao anatarajiwa kugombea urais.
Wandani wake pia walisema kwamba amegundua kwamba ngome yake itanufaika na baadhi ya mageuzi yanayopendekezwa kama vile maeneo mapya ya ubunge.
Rift Valley itapata maeneobunge 23 mapya miongoni mwa 70 yaliyopendekezwa ikilinganishwa na matatu katika ngome ya mpinzani wake mkuu Bw Odinga ya Nyanza.
Mnamo Ijumaa alishangaza wengi alipoashiria kwamba hatapinga mswada huo akisema mengi ya masuala aliyolalamikia yalishughulikiwa.
“Kifungu kipya 11A katika mswada wa kubadilisha katiba kupitia BBI kilichowekwa baada ya mkutano wa Bomas kitahakikisha uchumi wa mahsla wanaoendesha mikokoteni, bodaboda, mama-mboga, wafugaji, wauzaji wa bucha, sukari na mahindi wanalindwa,” Dkt Ruto aliandika kwenye ujumbe wa Twitter.
Kwa miaka miwili tangu Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani, Bw Odinga walipoasisi mchakato wa kubadilisha katiba, Dkt Ruto alikuwa akizunguka nchini kukutana na makundi ya watu aliowashawishi kuwa unalenga kubuni nafasi za uongozi kwa watu wachache.
“Hatuhitaji kubadilisha katiba ili kubuni nafasi tano za uongozi kwa ajili ya watu wachache. Tunahitaji mdahalo mpana wa kitaifa kuhusu jinsi ya kufaidi mahsla, ili waweke ‘mkate’ mezani,” alikuwa akisema katika mikutano aliyokuwa akiandaa kote nchini.
Mikutano yake ilikuwa ikivutia idadi kubwa ya vijana waliochangamkia misaada na ahadi alizowapa na mara kwa mara alikosoa polisi kwa kumnyima kibali cha kuiandaa.
Dkt Ruto alifaulu kushawishi viongozi wa kidini na baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakikosoa mchakato huo.
Alitaja juhudi za kubadilisha katiba kama kuharibu pesa za umma na kusema kuwa kinachohitajika ni kuinua maisha ya masikini na kuweka sera za kuinua maisha yao.
Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwisho iliyokusanya maoni kutoka kwa umma, Dkt Ruto alizomwa na wajumbe kwa kusisitiza kuwa haikutilia maanani maslahi ya walala-hoi na mwenendo wa ‘mshindi (wa urais) kujinyakulia kila kitu’.
Aidha, alikwepa kuwasilisha maoni yake kwa jopokazi lililoteuliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga na wakati mmoja alisema lilikuwa likiharibu pesa za umma kwa kuzunguka nchini kukutana na umma.
Alipokosa kuhudhuria uzinduzi wa ukusanyaji saini za kuunga mswada wa kubadilisha katiba kupitia BBI, wafuasi wake walitarajia kuwa angetimiza ahadi yake ya kusimama nao na kuendelea na kampeni yake ya kutetea maslahi ya wauzaji mboga, bodaboda na waendeshaji mikokoteni miongoni mwa makundi mengine ya mahasla.
Alipozomwa Bomas, Dkt Ruto alilalamika kuhusu kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu, kubuniwa kwa baraza la polisi na vyama vya kisiasa kuteua makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.
Wachanganuzi wanasema kwa kuamua kuunga mswada huo, amewaacha wafuasi wake wakiwa wamechanganyikiwa.
“Nilionya kuwa wanasiasa ni wale wale, wanahadaa ‘Wanjiku’ na kisha kuwaacha peke yao maslahi yao ya kibinafsi yakitimia,” alisema Njaga Wanjaga.
Anasema kwa kuunga mswada huo, Dkt Ruto ameunga juhudi za kubebesha mahsla mzigo zaidi wa kulipa idadi kubwa ya wabunge na watakaoshikilia nyadhifa mpya za uongozi zitakazobuniwa, BBI ikipitishwa kwenye refarenda.
Duru zinasema aliwaita wandani wake Ijumaa na kuwashangaza kwa kuwaarifu kwamba hatapinga mchakato huo.