BBI: Sahihi za kimabavu
Na WAANDISHI WETU
RAIA katika maeneo tofauti ya nchi wamelalamika kwamba maafisa wa utawala wa serikali kuu wanawalazimisha kutia sahihi za kuunga mkono marekebisho ya katiba.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika pembe mbalimbali za nchi umethibitisha kuwa, miongoni mwa wanaohangaishwa ni vijana, walemavu na wazee wanaotishiwa kutopewa huduma muhimu.
Hali hii inaonyesha taswira kwamba katiba itarekebishwa liwe liwalo, kwani katika mipango ya mapema, viongozi waliopinga mchakato huo waliadhibiwa hasa na vyama vya ODM na Jubilee.
Vijana waliohojiwa walifichua kwamba, wao hutishiwa na maafisa kama vile machifu na manaibu wao kuwa watanyimwa nafasi za Kazi Mtaani kama hawatakubali mswada wa marekebisho ya katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).
Kwa upande mwingine, wazee walidai kuambiwa hawatapokea pesa za msaada kutoka kwa serikali kama watakataa kutia sahihi kwenye vijitabu vya BBI. Ijapokuwa machifu na makamishna wengi wa kaunti walikana madai hayo, imethibitika kwamba walipewa viwango vya sahihi ambavyo kila mmoja anafaa kukusanya, na kuna wanaoogopa kumwaga unga endapo hawatafikisha viwango hivyo.
Katika baadhi ya maeneo, machifu na manaibu wao wanatembea kutoka boma moja hadi jingine wakitafuta sahihi za wapigakura.
Katika Kaunti ya Kisii, Bw David Kangwana alisema hajasoma ripoti ya BBI lakini alilazimishwa kutia sahihi ya kuunga mkono marekebisho ya katiba.
“Chifu wetu alikuja nyumbani kwangu akaniambia nitie sahihi kwenye fomu. Ijapokuwa sijawahi kuona ripoti ya BBI, nilitia sahihi kwa kuwa ninamheshimu,” akasema.
Machifu waliohojiwa na waandishi wetu waliomba wasitajwe wakisema wameambiwa wakusanye kati ya sahihi 200 hadi 400, kutegemea ukubwa wa maeneo wanayosimamia.
Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Kisii, Bw Abdirizak Jaldesa, serikali inalenga jumla ya sahihi 200,000 eneo hilo.
Katika kaunti ndogo za Moiben, Ainabkoi na Kapsereti zilizo Kaunti ya Uasin Gishu, vijana walisema kutokanana vitisho wanavyopokea, baadhi yao wamelazimika kutii amri na kuweka saini shingo upande.
“Mimi ilibidi niweke saini ili nisifukuzwe kazi kwani ni heri nitetee mahali ambapo napata unga kuliko kukaidi amri na nipoteze kazi,” alisema kijana mmoja mtaani Cylus mjini Eldoret.
Katika mtaa wa Langas baadhi ya vijana walidai kuwa kuna watawala wa mtaa ambao wanahakikisha kuwa kabla waanze shughuli za usafi mtaani, ni sharti waweke saini kwenye stakabadhi hyo.
Hali ilidaiwa kuwa hivyo katika mtaa wa Munyaka miongoni mwa mitaa mingine. Hata hivyo Chifu wa Chepkoilel, Bw William Sang alisema hakuna mtawala yeyote ambaye analazimisha vijana kusaini nakala hizo.
“Sijasikia kama kuna mtu yeyote ambaye amelazimishwa kuweka saini kwenye BBI. Huo ni uongo mtupu na propaganda za kisiasa,” alisema Bw Sang.
Wakazi katika eneo la Tudor mjini Mombasa walidai kuwa machifu walitishia kuwapokonya walemavu ufadhili wa serikali iwapo hawatia saini za kuunga mkono BBI.
Hata hivyo, machifu walipinga madai hayo wakisema kuwa ni mipango ya kuidunisha ripoti hiyo.
“Hakuna mtu aliyeshurutishwa kutia saini. Walioshiriki katika shughuli hiyo walifanya hivyo kwa kupenda kwao. Iwapo kuna mtu aliyetishiwa basi ana haki ya kupiga ripoti,” akasema Mohammed Musa, chifu wa Mwembe Tayari.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw Gilbert Kitiyo alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema hana ufahamu wa madai hayo. Wazee katika Kaunti ya Kakamega walilalamika kwamba machifu na manaibu wao wanatishia kuondoa majina yao kwenye orodha ya wanaopokea misaada ya fedha kutoka kwa serikali, kama watakataa kutia sahihi. Kwa upande mwingine, imesemekana kuwa wazee ambao bado hawajaanza kupokea fedha za msaada wanaahidiwa majina yao yatajumuishwa mara moja wakitia sahihi.
Mtetezi wa haki za binadamu katika Kaunti Ndogo ya Kakamega Mashariki, Bw Aggrey Majimbo, alisema wamepokea malalamishi mengi kutoka kwa wanavijiji.
Wazee wa vijiji na maafisa wa makundi ya Nyumba Kumi katika kaunti hiyo walilalamika kuwa wanafanya juhudi nyingi kupata sahihi ilhali hawalipwi chochote.
Katika kaunti ndogo kama vile Molo, Kuresoi Kaskazini na Kusini, Rongai, Subukia na Mogotio, zilizo katika Kaunti ya Nakuru, maajenti wa serikali wanaendesha shughuli hiyo nyumba kwa nyumba haswa masaa ya asubuhi na jioni.
Mratibu wa serikali katika eneo la Rift Valley, Bw George Natembeya, alisema wakazi hufunzwa kuhusu mswada wa BBI kabla kujiamulia kutia sahihi.
“Tuligundua kuwa wakazi wengi wa mashinani hawana ufahamu kuhusu mswada huu na ndiposa maajenti wakachaguliwa kuwasaidia kuelewa,” akasema.
Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o, hata hivyo alitetea kuhusishwa kwa maafisa wa utawala katika mchakato mzima wa ukusanyaji sahihi. Akieleza kuhusu mwelekeo huo, alithibitisha kuwa maafisa wa utawala wakiwemo machifu walipewa vitabu vya kukusanya sahihi za wanaounga mkono BBI.
“Inafaa ieleweke kwamba mchakato huu hauna maafisa kama vile wa IEBC ambao pengine wangetegemewa kuhifadhi vitabu vya kukusanya sahihi za wapigakura,” akasema alipohojiwa kwenye runinga Jumanne.