BBI: Uhuru na Raila wabanwa
Na WAANDISHI WETU
SHINIKIZO zinazotaka Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga waeleze wazi sababu yao halisi ya kutaka Jopo la Maridhiano (BBI) lifanye vikao kwa mara ya pili kitaifa, ziliendelea kutolewa Jumapili.
Ijapokuwa wawili hao husisitiza kwamba mpango huo umenuia kuwapa raia nafasi ya kuamua jinsi ya kutekelezwa kwa ripoti ya BBI iliyotolewa majuzi, viongozi mbalimbali wa kisiasa na kijamii wanadai kuwa kuna njama fiche ambayo wawili hao hawataki kueleza.
Baraza la Wazee la Jamii ya Wakalenjin (Myoot) lilieleza kuwa linahofia uwepo wa njama fiche kwenye ripoti hiyo. Baraza hilo lilisema kuwa kufikia sasa, halifahamu mpango uliopo kuihusu.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw James Lukwo, wazee hao walisema kuwa inavyoonekana, baadhi ya wanasiasa walisema kweli kwamba lengo la ripoti hiyo ni kubuni nafasi za kisiasa ili kutimiza malengo ya kibinafsi Rais Kenyatta na Bw Odinga.
“Fedha nyingi tayari zilitumika kwenye mchakato huo na kisha jopo hilo limeongezwa muda wake. Kinaya ni kwamba tungali tunaishi katika hali ya umaskini,” akasema.
Ijumaa iliyopita, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen, alisema kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wanapaswa kueleza wazi lengo lao katika ripoti hiyo kuliko kuwazungusha Wakenya.
Akihutubu Ijumaa kwenye mazishi ya mama yake Seneta Moses Kajwang (Homa Bay), Bw Murkomen alisema kuwa wawili hao wanapaswa kuweka wazi mpango wao.
“Haya masuala ya kubadilisha katiba hayajawekwa vizuri. Wewe (Odinga) na Rais Kenyatta mnataka nini kwenye ripoti ya BBI? Mnataka mfumo wa bunge, rais mwenye mamlaka mengi ama mchanganyiko? Semeni. Acheni kutuzungusha. Tuambieni ili tuipitishe bila kuwapotezea muda Wakenya,” akasema Bw Murkomen katika mazishi yaliyohudhuriwa pia na Bw Odinga.
Kauli kama hiyo imetolewa na mbunge Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) anayedai kwamba viongozi hao wawili wanalenga kutimiza ajenda zao fiche kwa kuliongezea muda jopo hilo.
“Ilivyo sasa, ripoti iliyotolewa ilikuwa jaribio tu. Wao wana ripoti halisi ambayo wanataka kuwashinikiza Wakenya kuipitisha. Hiyo ndiyo sababu kuu ambapo waataka vikao vingine kuandaliwa, ambapo watu wachache watateuliwa kuendesha mchakato huo,” akasema Bw Dawood kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Bw Dawood alisema kuwa mabadiliko yanayolengwa kufanywa hayanuii kuwafaa wananchi.
“Hatutaruhusu hilo kufanyika hadi pale watakapotwambia kuwa ripoti ya mwanzo ililenga kuwapumbaza Wakenya. Vikao vingine vitaigharimu nchi pesa nyingi na vitaendeshwa kwa maagizo ya watu wachache,” akasema.
Mbunge wa Mogotio, Bw Daniel Tuitoek alisema ni kinaya kwamba viongozi walioipigia debe ripoti hiyo wamebadilisha msimamo wao.
“Wenye ripoti hiyo sasa wanaipinga wakisema haifai. Hatua hiyo si nzuri kwa nchi. Wakenya walitoa maoni yao ambayo yalinakiliwa na jopo. Kutakuwa na faida gani kuandaa kura ya maamuzi?”
Wiki iliyopita, Bw Odinga alisisitiza kwamba uamuzi wa mwisho kuhusu BBI utatolewa na wananchi wala si viongozi wakuu wa kisiasa.
Ripoti za Wanderi Kamau, Gitonga Marete, Oscar Kakai na Samuel Baya