BBI yafufua mjadala wa siasa za majimbo Pwani
Na CHARLES LWANGA
MPANGO wa Maridhiano (BBI) umeanza kubadilisha siasa za eneo la Pwani baada ya mahasidi wa kisiasa kutoka vyama vya Jubilee na ODM kuweka tofauti zao kando na kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
Hasa, viongozi hao wameungana kusisitiza kuwa Kenya inapaswa kukumbatia mfumo wa utawala wa majimbo.
Katika kongamano la BBI mnamo Januari mjini Mombasa, Gavana wa Kilifi Amason Kingi ambaye aliwasilisha pendekezo la serikali ya mfumo wa majimbo kwa niaba ya magavana wote wa Pwani, wanataka Pwani igawanywe na kuwa majimbo mawili.
Gavana Kingi na wenzake Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kwale), Granton Samboja (Taita Taveta), Dadho Godhana (Tana River) na Gavana Fahim Twaha wa Lamu, waliwasilisha mapendekezo 16 wakidai yatatatua dhuluma za kihistoria za ardhi na kuimarisha uchumi wa Pwani.
Viongozi wa Pwani wamekuwa wakiunga mkono mapendekezo hayo ya BBI yaliyowalislishwa na magavana isipokuwa wale wa kundi la Tangatanga hadi wiki iliyopita ambapo mbunge wa Kilifi Kaskazini alipinga pendekezo hilo akidai ni la kibinafsi na lenye njama kuundia baadhi ya viongozi nafasi za kimamlaka.
Wiki jana, Gavana Kingi alisema kuwa ndoto ya Wapwani kuunda serikali ya majimbo ambayo itakuwa na mikoa huku ikibakisha zile za kaunti kupitia kwa ripoti ya BBI haitazimwa wala kufifia.
Bw Kingi pia aliwakashifu wanaopinga BBI ambayo pia inapendekeza uundaji wa kiti cha waziri mkuu na naibu wake akisema pendekezo hilo linasimamia maoni ya Wapwani na ya Wakenya wote.
Akihutubia wakazi eneo la Jibana katika eneobunge la Kaloleni ambapo alizindua hospitali ya wajawazito, alisema wito wa uundaji wa serikali ya majimbo ni wa tangu nyakati za ukoloni.
“Serikali ya wakati huo ilitekeleza mfumo wa majimbo na baadaye mfumo huo ukabanduliwa mwaka mmoja baada ya uhuru,” alisema.
Bw Kingi alisema wakati huu wakazi wa Pwani wana nafasi nyingine ya kusukuma mfumo wa majimbo kupitia kwa BBI ambayo kutimizwa kwake kulikuwa kumefeli tangu ipendekezwe na Bw Ngala.
‘Taifa Jumapili’ imebaini kuwa Waziri Msaidizi wa Ardhi, Bw Gideon Mung’aro ambaye ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa Jubilee eneo la Pwani, huenda akajiunga na ODM pamoja na wafuasi wake kutokana na maridhiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Raila Odinga.