Habari

Bodaboda wa Kitengela nusra azirai kupata mteja aliyeitiwa gesti ni mkewe

Na CORNELIUS MUTISYA December 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWENDESHAJI bodaboda nusra apoteze fahamu alipopigiwa simu akabebe mteja katika gesti, na kupata ni mkewe ametoka kula uroda na jamaa.

Kulingana na mdokezi, boda huyo ni maarufu sana mjini Kitengela katika Kaunti ya Kajiado na watu wengi walikuwa na namba yake ya simu na hivyo huwa anaitwa kubeba wateja.

Juzi, alirauka alfajiri kuchapa kazi na akamuacha mkewe akitekeleza majukumu ya nyumbani kama ilivyokuwa kawaida yake.

Inadaiwa kuwa saa mbili usiku alipigiwa simu na mhudumu wa gesti moja mjini akabebe mteja.

Hata hivyo, alishtuka sana alipopata mteja huyo alikuwa ni mkewe aliyekuwa ameandamana na jamaa kibonge asiyemfahamu.

Mke alipomuona ilikuwa ni mguu niponye akatoroka kama pepo. Naye bodaboda akaenda zake huku amefura kwa hasira.