Habari

Buhari amshinda mpinzani wake mkuu kwa zaidi ya kura 4 milioni

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ABUJA, NIGERIA

RAIS Muhammadu Buhari ameshinda urais muhula wa pili ambapo ataongoza tena taifa hili lenye idadi kubwa ya watu katika Bara la Afrika; yanaonyesha matokeo ambayo bado tume ya uchaguzi haijayatangaza rasmi.

Raia wasimama palipo na bango la mgombea wa chama cha All Progressives Congress (APC) Rais Muhammadu Buhari mara baada ya kuchaguliwa tena Abuja, Nigeria Februari 26, 2019. Picha/ AFP

Mapema Jumatano tume ya uchaguzi imetangaza kwamba Buhari yuko kifua mbele kwa zaidi ya kura 4 milioni dhidi ya mpinzani wake mkuu ambaye pia aliwahi kuwa makamu wa Rais, Atiku Abubakar, ishara kwamba kiongozi wa nchi hakamatiki.

Upinzani mnamo Jumanne ulipuuzilia mbali matokeo hayo, ukidai kulikuwa na udanganyifu hata kabla ya matokeo ya majimbo 36 kutangazwa.

Chama cha Atiku cha People’s Democratic Party (PDP) kiliitisha kikao na wanahabari kikiitaka tume ya uchaguzi kusitisha ujumuishaji wa kura.

Afisa wa PDP, Tanimu Turaki alisema uchakachuaji wa kura ulifanyika.

“Chama cha PDP kinashikilia kwamba kura zilizopigwa vituoni na ambazo tunazo, zinaonyesha raia wa Nigeria kwa uwazi kabisa walimchagua Atiku Abubakar,” alisema Turaki.

Aidha PDP kinasema kinataka kura kupigwa upya katika majimbo matatu.

Hadi kufikia Jumanne asubuhi, Rais Buhari alikuwa ameshinda katika majimbo 36, huku mpinzani wake Atiku Akubakar akishinda katika majimbo mawili na Jiji Kuu la Abuja.

Mwenyekiti wa PDP, Uche Secondus alitaja shughuli ya kuhesabu kura kuwa “isiyo sahihi na isiyokubalika” akiongeza kuwa kumekuwa na “jaribio la serikali na mashirika mengine kubadili matokeo.”

Mashirika ya EU, AU na US yameeleza kughadhabishwa kwake na kucheleweshwa kwa shughuli hizo, japo hakuna kati ya waangalizi wa uchaguzi huo wametaja lolote kuhusu wizi wa kura kwenye uchaguzi huo.

Chama

Rais Buhari ni wa chama cha All Progressives Congress (APC).

Vyama vyote viwili vimelaumiana kuwa kingine kinashirikiana na tume ya uchaguzi nchini humo (Inec) ili kuiba kura.

Uchaguzi huo ulifaa kufanywa mnamo Februari 16 lakini ukaahirishwa, saa tano kabla ya uchaguzi kuanza.

Mshindi ana kibarua kigumu katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika na pia lenye utajiri mkubwa, cha kutatua matatizo ya umeme, ufisadi, mavamizi ya kigaidi nay a kiuchumi.

Hata hivyo, matokeo kamili ya uchaguzi huo yatatolewa mwishoni mwa wiki hii.

Wagombeaji waliosajiliwa ni 73. Washindani wakuu, hata hivyo walikuwa ni Buhari na Abubakar ambao wanatoka kaskazini mwa taifa hilo na ambao wote wana zaidi ya umri wa miaka 70.

Wakati huo huo, polisi nchini hume walisema kuwa waliwakamata watu 128 kwa kutuhumiwa kuhusika na makossa ya uchaguzi, yakiwemo wizi wa masanduku ya kupigia kura, kuhongana katika maeneo ya kupiga kura na kujifanya kuwa watu wengine.

Polisi aidha walisema kuwa vilipuzi pamoja na silaha nyingine zilipatikana katika maeneo ya kupiga kura.

Uchunguzi mwingine ulisema kuwa watu 39 wameaga dunia katika visa vya fujo za uchaguzi nchini humo, kikiwemo cha vamizi la kigaidi kaskazini mashariki mwa taifa hilo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Mahmood Yakubu aidha alisema kuwa japo uchaguzi umeendeshwa kwa njia salama, mmoja wa wafanyakazi wake aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akitoka kuendesha uchaguzi.

Watu milioni 72 walisajiliwa kupiga kura.