Habari

Bunge la kaunti kulipa aliyenyimwa kazi Sh7 M

Na SAM KIPLAGAT November 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BUNGE la Kaunti ya Nairobi imeamriwa kumlipa Bw Halkano Dida Waqo, fidia ya Sh7 milioni baada ya kuhojiwa kwa wadhifa wa Afisa Mkuu wa Kaunti mwaka jana, lakini jina lake likakosa kuidhinishwa bila sababu wala maelezo yoyote.

Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi iliamua kuwa Bunge la Kaunti na Spika wake hawakumtendea haki Bw Waqo, kwani walimfanya kusubiri kwa muda mrefu bila kumjulisha matokeo ya mchakato wa uteuzi wake.

Jaji alisema Bw Waqo alipitia “mateso makubwa” baada ya mchakato wa uteuzi wake kuvurugika bila maelezo, na kwamba hatua hiyo ilikiuka haki zake za kikatiba.

“Ili kufidia ukiukaji huo, mlalamishi anatunukiwa Sh7,000,000, zitakazolipwa kwa pamoja au kibinafsi na serikali ya kaunti na Spika,” ilisema mahakama, ikiongeza kuwa kiasi hicho lazima kilipwe kufikia Januari 2026, la sivyo kitaanza kutozwa riba.

Bw Waqo alithibitisha alikuwa miongoni mwa maafisa saba walioteuliwa Aprili mwaka jana kwa nyadhifa mbalimbali za maafisa wakuu wa kaunti. Baada ya majina yao kutangazwa, wananchi waliombwa kuwasilisha maoni kabla ya majina hayo kupelekwa bungeni kwa mchakato wa kuidhinishwa.

Hata hivyo, wakati Bunge la Kaunti lilipoketi Mei mwaka jana kuzingatia ripoti za kamati mbalimbali, jina la Bw Waqo halikuwemo kwenye ripoti ya kamati ya Ardhi, Mipango na Makazi, licha ya yeye kufanyiwa kukaguliwa rasmi.

Bw Waqo alisema kuwa hakuwahi kufahamishwa kama jina lake lilikubaliwa au kukataliwa, jambo alilosema lilimnyima haki yake ya kujua hatma ya ajira aliyoitarajia. Alidai kuwa kutokana na kusubiri ajira hiyo, hakutafuta kazi nyingine kiuchumi au kitaaluma.

Mnamo Septemba mwaka jana, aliandika barua kwa Bunge la Kaunti akiomba maelezo kuhusu hatima ya uteuzi wake, lakini hakupata majibu yoyote.

Mahakama ilisema hatua ya Bunge kutomjulisha matokeo ya mchakato huo ilisababisha maumivu ya kihisia, msongo wa mawazo, na hasara ya kiuchumi, ikiwemo kupoteza heshima ya kitaaluma na fursa za kazi.