Habari

Bunge lawapa Wakenya majuma mawili kutoa maoni kuhusu Mswada wa Fedha 2025

Na CHARLES WASONGA May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BUNGE la Kitaifa limetoa muda wa majuma mawili kwa Wakenya kutoa maoni, mapendekezo au pingamizi kuhusu Mswada wa Fedha wa 2025, ambao serikali inadai haujapendekeza nyongeza ya ushuru kukwepa kero za Gen Z.

Watu binafsi na wadau mbalimbali wako na nafasi ya hadi Mei 27 kuwasilisha maoni yao, kwa Karani wa Bunge au Kamati ya Bunge kuhusu Fedha kwa njia ya taarifa au watume barua pepe; [email protected] au [email protected].

Vile vile, Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani inatarajiwa kuandaa vikao sehemu mbalimbali nchini kushirikisha maoni kutoka kwa umma.

Kile Wizara ya Fedha imefanya ni kwamba haijapendekeza nyongeza ya viwango vya ushuru. Lakini haijasema ni vipi inawasaidia Wakenya wanaolalamikia kupungua kwa mapato yao, haswa mishahara, kila mara – Philip Muema, mtaalamu wa masuala ya bajeti

Hii ni licha ya kwamba Wakenya wamekuwa wakilalamika kuwa wabunge hupuuza maoni yao kuhusu mswada huo huku wakizingatia na kupitisha mapendekezo yanayofikia na matakwa ya Serikali Kuu.

Kulingana na wao, wabunge hutumia tu vikao vya kushirikishaji wa umma kutimiza matakwa ya kipengele cha 118 cha Katiba ya sasa wala si kwa lengo la kuzingatia matakwa ya Wakenya.

Ni malalamishi kama hayo yaliyochangia vijana wa Gen Z kufanya maandamano kote nchini Juni mwaka jana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 wakidai wabunge walishawishiwa na Ikulu kupuuza matakwa ya Wakenya na kupitisha mapendekezo ya Serikali Kuu.

Kilele cha maandamano hayo kilikuwa uvamizi wa majengo ya bunge mnamo Juni 25, 2024 ambapo vijana kadhaa waliuawa na polisi, mamia kujeruhiwa, wengine kutekwa nyara na mali ya thamani kubwa kuharibiwa.

“Mswada huu unasheheni mapendekezo yanayohusiana na hatua za kukusanya mapato, ikiwemo yale ya kurahisisha usimamizi wa ushuru na mapendekezo mengine yanayohusiana na upanuzi wa mawanda ya ukusanyaji ushuru,” akasema Karani wa Bunge Samuel Njoroge katika tangazo hilo la kuwaalika Wakenya kuwasilisha maoni kuhusu mswada huo unaolenga kuisaidia serikali kukusanya fedha zao za kufadhili shughuli zake.

Licha ya kwamba Mswada wa Fedha wa 2025 haujapendekezi nyongeza ya ushuru au kuanzishwa ushuru mpya, baadhi ya mapendekezo yaliyomo yanaweza kuchangia kupanda kwa gharama ya maisha.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni kama vile; kuondolewa kwa baadhi ya bidhaa kutoka orodha ya zile ambazo watengenezaji wazo wanaruhusiwa kudai ushuru wa VAT hadi zile ambazo watengenezaji hawarejeshewi VAT wanayolipa kwa malighafi ya kuzitengeneza.

Miongoni mwa bidhaa hizi ni malighafi yanayotumiwa na watengenezaji dawa, dawa za kuangamiza wadudu wanaoathiri mimea shambani na lishe ya mifugo.

Aidha, mswada huo umeanzisha ushuru wa VAT kwa usafirishaji wa miwa kutoka mashambani hadi viwandani, mabasi, pikipiki na baiskeli zinazotumia umeme na betri za vifaa vya kuzalisha kawi kutokana na jua (sola).

Endapo mapendekezo hayo yatapitishwa na wabunge, gharama ya uzalishaji wa mazao ya shambani itapanda hali ambayo itachangia kupanda kwa bei ya bidhaa hizo.

Aidha, bei ya mabasi na pikipiki zinazotumia umeme zitapanda, hali itayopunguza kasi ya watu kununua magari ya umeme na hivyo kuathiri juhudi za serikali za kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Aidha, mtaalamu wa masuala ya ushuru Philip Muema anasema Mswada wa Fedha wa 2025 haujashirikisha mapendekezo ya kutoa afueni kwa Wakenya wanaolalamikia “ufinyu wa mapato yao”.

“Kile Wizara ya Fedha imefanya ni kwamba haijapendekeza nyongeza ya viwango vya ushuru. Lakini haijasema ni vipi inawasaidia Wakenya wanaolalamikia kupungua kwa mapato yao, haswa mishahara, kila mara. Kwa upande mwingine Wizara inakusudia kukusanya Sh175 bilioni kupitia mapendekezo kadhaa kwenye mswada huo,” akaeleza mtaalamu huyo kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne usiku.