Habari

Cha maana ni matumizi mazuri ya fedha zinazopelekwa kwa kaunti – mbunge

August 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

FEDHA za mgao zinazotumwa kwa kaunti tofauti zinastahili kutumika kwa njia nzuri na wanaozisimamia wahakikishe zinawafaa wakazi, amesema mbunge.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema hata ingawa kaunti nyingi zinataka serikali kuu iziongeze kiwango zaidi cha fedha, ni vyema kutumia vyema zile ambazo zimetumwa.

Alisema hata kaunti zinazopigania kupata mgao zaidi zinastahili pia kuonyesha umma ni nini wamefanya na fedha walizopewa na serikali kuu.

Iwapo serikali kuu inatoa fedha katika kaunti tofauti ni vyema kuzingatia wingi wa watu ili kuonyesha usawa kamili.

“Hakuna kaunti inayostahili kunyanyaswa kuhusiana na ugavi wa fedha hizo lakini wapate kile kilicho chao,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano eneo la Mang’u, alipohudhuria mazishi ya mkazi mmoja wa kijiji cha Igegania.

Alisema fedha za ushuru zinazopatikana katika kaunti tofauti zikitumiwa vizuri zitaleta mabadiliko mkubwa katika kaunti nyingi hapa nchini.

Alieleza kuwa fedha nyingi za kaunti huwa hazitumiki vyema inavyostahili ambapo utapata kaunti nyingi zikiwa bado nyuma kimaendeleo.

“Lengo la ugatuzi lilikuwa njema baada ya katiba kuzinduliwa, ambapo ilinuia kumjali mwananchi wa kawaida. Lakini usimamizi mbaya wa fedha imesababisha kaunti nyingi kutatizika kimaendeleo,” alisema Bw Wainaina.

Alisema viongozi waliopewa mamlaka wakiwajibika ipasavyo, bila shaka lengo la ugatuzi litatimia.

Alisema kila kaunti ipewe fedha zinazowafaa bila kunyanyaswa, lakini maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu pia ipewe haki yake.

“Kile cha muhimu mwananchi wa kawaida anahitaji ni kupata maendeleo. Hayo yakitendeka bila shaka kila kaunti itakuwa na jambo la kujivunia,” alisema mbunge huyo.

Alisema malumbano ambayo yameshuhudiwa katika bunge la seneti kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha katika kaunti yanastahili kufika kikomo haraka iwezekanavyo ili fedha zisambazwe mara moja katika kaunti hizo.