Chebukati awajibu wabunge wa ODM wanaolalama
Na CHARLES WASONGA
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, amejibu madai ya wabunge wa ODM kwamba tume hiyo inapanga kuvuruga sajili ya wapigakura wa Kibra.
Amepuuzilia madai hayo akiyataja yasiyo ya kweli, akishilikia kuwa sajili hiyo ni salama.
Kwenye ujumbe katika ukurasa wa akaunti ya Twitter ya tume hiyo, Bw Chebukati anasema kuwa baada ya kiti hicho kutangazwa wazi kufuatia kifo cha marehemu Ken Okoth usajili wa wapigakura ulisitishwa.
“Lakini kabla ya hapo, wapigakura 333 zaidi walijiandikisha kama wapigakura katika eneo la Kibra sawa na eneobunge lingine nchini. Hii kwa sababu shughuli hiyo huendelea kila wakati,” akasema Bw Chebukati.
Akaongeza: “Kwa hivyo, ningependa kuwahakikishia wanaolalamika kuwa sajili hiyo iko salama na haijavurugwa kwa njia yoyote.”
Bw Chebukati alieleza kuwa idadi ya watu waliohamisha kura zao kutoka maeneo bunge mengine hadi Kibra ilikuwa ni 44 huku wale waliobadilisha vituo vyao vya kupigia kura ndani ya eneobunge hilo ni 22.
“Jina la mpigakura mmoja lilifutiliwa mbali na jina la mwingine likaingizwa kwenye sajili rasmi baada ya hitilafu kuondolewa,” akaongeza Bw Chebukati.
Sajili
Hata hivyo, tume hiyo ilikubali kuwa ilipokea barua mbili kutoka ODM; chama hicho kikitaka kipewe sajili ya wapigakura.
Hata hivyo, Bw Chebukati hakueleza ni kwa nini tume hiyo haikutoa maelezo ambayo chama hicho kilitaka wakati huu, mwezi wa Septemba, ilhali usajili wa wapigakura wapya ulisitishwa mnamo Agosti 6, 2019.
Mnamo Jumanne, wabunge 10 wa ODM wakiongozwa na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed walitangaza kuwa Jumatano wataandamana hadi makao makuu ya IEBC jumba la Anniversary Towers kuitisha sajili hiyo.
Wabunge hao walidai wanashuku kuwa tume hiyo inapanga kuvuruga sajili hiyo kwa lengo la kufanikisha udanganyifu katika uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Novemba 7, 2019.
“Kibra ni ngome ya ODM na hatutaruhusu IEBC kuichezea kwa kujaribu kuendesha hila za kubadili sajili ya wapigakura. Tunaitaka tume hii kutoa sajili hiyo au iichapishe wazi katika kurasa za mtandao na tovuti yake kama inavyotakikana kisheria,” akasema Bw Mohamed ambaye pia ndiye mkurugenzi wa uchaguzi katika ODM.