HabariSiasa

Corona haitambui mamlaka, waliokuwa Ikulu kupimwa

June 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

UKWELI kuwa virusi vya corona havitambui mamlaka wala tabaka ulidhihirika Jumatatu baada ya kuthibitishwa kuwa maambukizi yamefika katika Ikulu ya Nairobi.

Tangu kisa cha kwanza cha maambukizi kutangazwa nchini mnamo Machi, Rais Uhuru Kenyatta amesimamia mikutano mingi ya viongozi katika ikulu hiyo ambapo huwa anaishi na familia yake.

Kulingana na taarifa kutoka ikulu hiyo, watu wanne walipatikana kuambukizwa wakati walipopimwa Alhamisi iliyopita.

Hii ni licha ya masharti tele ambayo kila mmoja anayetaka kuingia ikuluni huhitajika kufuata ili kuepusha maambukizi katika eneo hilo lililo na ulinzi mkali.

“Kila mmoja hupimwa mara kwa mara ikiwemo Rais na familia yake. Wiki iliyopita mnamo Alhamisi, Juni 11, 2020, watu wanne walipatikana wameambukizwa,” akasema msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena kupitia taarifa kwa vyumba vya habari.

Hata hivyo, haikubainika kama ni wafanyakazi au wakuu wa serikali wanaomhudumia Rais, ambao waliambukizwa.

Bi Dena aliongeza kuwa wagonjwa hao walilazwa katika Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta katika Kaunti ya Kiambu, huku waliotangamana nao wakisakwa ili wapimwe.

Kufikia jana, idadi ya maambukizi kitaifa iliongezeka kwa watu 133, na kufikisha jumla ya watu 3,737 walioambukizwa.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alisema watu wengine 33 walipona na kufikisha idadi yao kuwa 1,286. Hata hivyo, mmoja mwingine alifariki.

Mkutano wa mwisho uliofanywa Ikuluni ilikuwa mnamo Juni 1, wakati wa sherehe za Madaraka Dei.

Kutokana na kanuni za kuepusha ueneaji virusi vya corona, sherehe hizo ambazo zilikuwa zimepangiwa kufanywa katika Kaunti ya Kisii hazingeandaliwa kama ilivyo kawaida uwanjani na kuhudhuriwa na umati wa wananchi.

Miongoni mwa viongozi ambao walikuwa Ikuluni kwa sherehe hizo ni Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, na Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Robert Kibochi.

Wengine waliokuwepo ni mawaziri kadhaa akiwemo Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i.

Wabunge na maseneta waliwakilishwa na viongozi wao, akiwemo Kiongozi wa Wengi wa Seneti, Bw Samuel Poghisio na mwenzake wa Wachache James Orengo.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya na Gavana wa Nairobi Mike Sonko pia walikuwepo.

Mama wa Taifa, Bi Margaret Kenyatta na mkewe Naibu Rais, Bi Racheal Ruto walihudhuria lakini wakakaa barazani katika orofa ya juu, mbali kutoka kwa umati uliokuwa katika bustani ambapo hafla iliandaliwa.

Siku iliyofuata, Rais alisimamia kikao cha wabunge na maseneta wa Jubilee ambacho pia kilihudhuriwa na Dkt Ruto pamoja na viongozi 212 wa chama.

Tangu wakati huo, kumekuwa na mikutano mingine kadhaa ya kiserikali ambayo huhudhuriwa na mawaziri na viongozi wakuu serikalini.

Jana, Bw Odinga alithibitisha kwamba hajaambukizwa virusi vya corona na akatoa wito kwa wananchi wengine waende kupimwa ili wajue hali yao wasije wakaambukiza wenzao.

Bw Odinga alikuwa ameenda kupimwa virusi hivyo mnamo Jumapili katika kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Kenya (Kemri) iliyo Mbagathi, Nairobi.

“Nawasihi Wakenya wapimwe, watumie vieuzi na wasitangamane na wenzao,” akasema Bw Odinga.

Ikulu ilithibitisha kuwa, Rais Kenyatta na familia yake pia walipimwa na ikabainika hawajaambukizwa virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

“Tunakumbusha Wakenya kuwa kila mtu yumo hatarini kuambukizwa ugonjwa huu. Hakuna mtu ambaye hawezi kuambukizwa. Kwa hivyo tujitahidi kufuata kikamilifu kanuni zote zinazolenga kudhibiti Covid-19 jinsi zilivyotangazwa na Wizara ya Afya,” akasema Bi Dena.

Alieleza kuwa familia za wanne hao zinafuatiliwa kwa karibu, na vilevile watu wote waliotangamana nao kwa karibu.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwepo Ikuluni kwa muda huo wote, hasa mawaziri na wabunge, hutangatanga katika sehemu tofauti za nchi wakidai ni harakati za kukagua miradi ya maendeleo.

Hii ni licha ya Wizara ya Afya kutoa kanuni za kuzuia watu kusafiri ndani na nje ya Nairobi kwa sababu ya idadi kubwa ya maambukizi ya corona katika jiji hilo kuu.