Habari

CORONA: Maskini Nairobi kulipwa na serikali

April 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WAKAZI wa jiji la Nairobi wasiojiweza kimapato watapokea msaada wa kifedha kila wiki kutoka kwa serikali kuu, kuwasaidia wakati huu wanapotaabika kutokana na athari za janga la corona.

Maelfu ya wananchi wanashindwa kujitafutia riziki kutokana na masharti makali ya kupambana na virusi hivyo, kama vile maagizo ya kutokaribiana, kafyu na vikwazo vya usafiri. Kwa sasa vibarua wengi wamepoteza ajira huku biashara zikizotota.

Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi alitangaza hatua hiyo miongoni mwa nyingine ambazo zinalenga kuwapunguzia mzigo kwa wananchi kimaisha wakati huu taifa limo vitani dhidi ya virusi vya corona.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi, Rais alisema serikali imetoa jumla ya Sh8.5 bilioni kusaidia wananchi wazee na wale wenye mahitaji mazito.

“Tumetambua familia zilizo na mahitaji ambazo zitaanza kupokea fedha za msaada kila wiki. Shughuli hii ilianza jana (Jumatano) na kuna wale ambao tayari wamepokea zao,” akasema Rais.

Aliongeza kuwa, shughuli hiyo ilianza Nairobi kwa majaribio lakini itajumuisha taifa lote.

Hata hivyo, haikubainika mara moja vigezo vilivyotumiwa kuamua kuhusu familia zinazostahili kupokea misaada, wala kiwango cha fedha watakachopokea.

“Misaada itaendelea kutolewa kwa wananchi, taasisi na mashirika yaliyoathirika zaidi kwa janga hili la corona,” akasema.

Alitangaza pia serikali imetoa Sh500 milioni ambazo walemavu wamekuwa wakisubiri kwa muda.

Alhamisi, idadi ya walioambukizwa virusi vya corona ilifika 234 baada ya watu tisa zaidi kupatikana na virusi hivyo.

Idadi ya waliopona na kuruhusiwa kwenda nyumbani ni 53, lakini kuna watu 11 waliofariki kufikia jana.

Ingawa Rais Kenyatta alieleza matumaini kwamba, mikakati ya serikali kupambana na janga hilo lililotikisa ulimwengu inazaa matunda, alionya kuna hatari ya kupiga hatua nyuma endapo wananchi watalegeza kamba kwa masharti yaliyotolewa.

“Wakenya wenzangu, tuko na shida na hii shida sio yetu bali tuliletewa kutoka nje na inakumba karibu kila taifa duniani. Kuna wengi ambao wanachezea huu ugonjwa na wenzangu nataka niwaambie ugonjwa huu hauna mpaka wala haubagui kwa msingi wowote,” akasema Rais.

Aliongeza: “Sisi sote tuko hatarini ndiposa twasema ni jukumu la kila Mkenya kujikinga, kukinga wenzake, na familia yake ili hili janga lituondokee bila kuumiza au kuangamiza Wakenya wengi zaidi.”

Alionya wananchi dhidi ya kushambulia polisi ambao wanafuatilia utekelezaji wa masharti yaliyotolewa na serikali, lakini pia akataka polisi wasitumie nguvu kupita kiasi wanapokuwa kazini.

“Tunahitajika tushirikiane, tuendelee kuhakikisha Wakenya wanatii sheria lakini pia tufanye kazi yetu kwa njia ya huruma. Tusinyanyase Wakenya wenzetu ndipo waweze kutii bila kuwaumiza. Mwongeleshe ili ajue hatari ambayo anajiwekea yeye mwenyewe na wenzake,” akasema. Kando na hayo, Rais alitangaza kuwa Hazina ya Dharura ya Covid-19 imepokea zaidi ya Sh1 bilioni kutoka kwa wahisani.

Aliagiza Wizara ya Afya ibuni sera ambazo zitaepushia madaktari na wahudumu wa afya madhara wanapotibu wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona. Hii inajumuisha kuwepo bima maalumu kwa wahudumu hao.

Ili kupiga jeki juhudi za serikali za kaunti, aliagiza zizilipe madeni kwa Shirika la Kusambaza Dawa Nchini (Kemsa) kwa miezi mitatu ijayo, ili watumie fedha zao kwa mahitaji ya kupambana na janga lililopo kwa sasa.

Serikali za kaunti pia ziliongezwa Sh5 bilioni za kutoa misaada kwa umma na kununua vifaa ambavyo vinahitajika hospitalini, kwa sharti kwamba vifaa hivyo vitanunuliwa kutoka kwa viwanda vya humu nchini wala si kutoka nchi za nje.

Kuhusu hali ya uchumi inayohofiwa itaendelea kuzorota, Rais alisema kuna mikakati inaendelezwa kuhusu jinsi taifa litaepushwa kuathirika sana wakati huu na baadaye. Aliongeza kuwa, mashauriano yanaendelezwa na mataifa ya nje ili Kenya isihitajike kulipia madeni yake yaliyofika Sh6 trilioni kwa sasa ndipo ipate nafasi bora ya kujifufua kiuchumi.