Habari

CORONA: Mwanamke aliyetengwa kwa lazima 'ajitia kitanzi' Nakuru

March 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA ERIC MATARA

MWANAMKE wa miaka 27 kutoka nchini Afrika Kusini aliyekuwa ametengwa kwa lazima kwa siku 14 mjini Nakuru amepatikana amefariki chumbani mwake Ijumaa asubuhi.

Mwili wa Elizabeth Holloway ulipatikana ukining’inia kweny paa ya chumba hicho cha Taasisi ya Kitaifa ya Mafunzo ya Viwanda, maafisa walisema.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Nakuru Bw Gichuki Kariuki alithibitisha kisa hicho ila hakutoa taarifa zaidi.

Wahudumu wa afya, ambao walienda kwa chumba hicho katika harakati zao za kila siku za kuwajulia hali waliotengwa walisema mwanamke huyo alijitia kitanzi akitumia kitambaa.

Ilibainika kuwa mwanamke huyo alikuwa amelalamikia mazingira mbovu ya chumba hicho hapo Alhamisi.

“Aliwaita maafisa wasimamizi akiomba kuhamishiwa mahali penye mazingira bora,” mtu mmoja ambaye hakutaka kutambuliwa aliambia Taifa Leo Dijitali.

Katika taasisi hiyo, alikuwa ametengwa pamoja na Wakenya watatu akiwemo mwanariadha wa Eldoret Samuel Ruto, ambaye alitua nchini hapo Jumamosi.

Waliotangamana na Bi Holloway kabla ya kifo chake walisema alikuwa binti mchangamfu aliyejawa na bashasha.