Corona yakoroga masomo
NA WANDERI KAMAU
WANAFUNZI wote wa shule za msingi na upili watalazimika kurudia madarasa mwaka ujao, baada ya serikali kufutilia mbali ratiba ya masomo mwaka huu kutokana na janga la corona.
Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, alitangaza pia kwamba, kutotokana na mashauriano baina ya wadau hakutakuwa na mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) mwaka huu.
Matumaini kwamba shule zingefunguliwa ifikapo Septemba, au angalau watahiniwa kuruhusiwa kurejea shuleni sasa yametokomea kwa kuwa maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kuongezeka, na yanatarajiwa kufika kileleni Septemba.
Taasisi za elimu ya juu pekee ndizo zitaanza kufunguliwa kwa zamu wakati huo, kwa mujibu wa waziri.
Akihutubu jijini Nairobi jana, Prof Magoha alisema maamuzi hayo ya Jopo Maalum la Wataalamu yalimridhisha Rais Uhuru Kenyatta.
“Maagizo haya yatafuatwa na shule zote. Watoto wote ni sawa humu nchini. Hakuna tofauti kati ya mtoto wa (shule ya) umma, kibinafsi wala kimataifa,” akasema Prof Magoha.
Wanafunzi waliokuwa wamesajiliwa kufanya mtihani wa KCSE mwaka huu ni 752,836 huku wale waliosajiliwa kufanya mtihani wa KCPE wakiwa milioni 1.2.
“Ikiwa tungeruhusu wanafunzi wa Darasa la Nane kufanya mtihani wa KCPE mwaka huu, ingemaanisha jumla ya wanafunzi 438,490 hawangepata nafasi katika Kidato cha Kwanza. Kando na hayo, ingekuwa vigumu kuhakikisha wanafunzi hawakaribiani, kulingana na kanuni zilizotolewa na Wizara ya Elimu ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona,” akasema Prof Magoha.
Alieleza kuwa, sababu nyingine ya kuahirisha mitihani ya kitaifa ni kwamba, ingekuwa vigumu kwa wanafunzi walio katika Darasa la Saba na Kidato cha Tatu kukamilisha mihula iliyobaki kwa muda mfupi uliosalia.
“Wanafunzi hao wamepoteza mihula miwili mwaka huu. Je, wangewezaje kukamilisha mihula hiyo katika mwaka 2021 pekee? Hilo halingewezekana,” akasema.
Sababu nyingine ya hatua hiyo ni kuwa, ikiwa wanafunzi wangeruhusiwa kusafiri kurejea katika shule zao kwa kuabiri magari, hilo lingewaweka kwenye hatari ya kuambukizwa na kusambaza virusi hivyo.
Hatua hii itakuwa pigo kwa walimu wa shule za kibinafsi na wale wanaoajiriwa na bodi za usimamizi wa shule ambao wengi wao hawajapokea mishahara tangu Machi. Wadau wa elimu waliozungumza katika kikao hicho cha wanahabari walieleza kuridhika na hatua hiyo ya serikali.
“Usalama wa watoto na walimu shuleni ni muhimu. Kwa hivyo, Wakenya wanafaa kuunga mkono uamuzi huu. Raia wote na wazazi hakikisheni watoto wakiwa nyumbani wako salama hadi wakati watarudi shuleni,” akasema Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Bw Wilson Sossion.
Kauli hii iliungwa mkono na mwenzake wa Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET), Bw Akello Misori ambaye alisisitiza kutakuwa na changamoto kubwa endapo maambukizi ya corona yatazidi watoto wakiwa shuleni.
Mwakilishi wa shule za kibinafsi katika kamati hiyo, Bi Mutheu Kasanga alisema mashauriano yataendelezwa kuhusu jinsi walimu wa shule za kibinafsi na wale wa bodi za usimamizi wa shule watakavyosaidiwa shule zikiwa zimefungwa.
Kuhusu vyuo vikuu na anwai, Prof Magoha alisema wizara hiyo itatoa mwongozo kuhusu tarehe ambapo taasisi hizo zitafunguliwa. Kulingana na waziri, Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) vilevile litatoa ratiba mpya kuhusu mitihani katika taasisi hizo.