Habari

COVID-19: Abiria jijini Nairobi wapewa jeli ya kusafisha mikono

March 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

BAADHI ya matatu yanayohudumu jijini Nairobi na viunga vyake yameanza kutekeleza utaratibu uliotolewa na serikali kwa umma ili kuzuia maambukizi ya COVID-19.

Kampuni kadha za uchukuzi zinazohudumu kati ya eneo la Githurai na Nairobi, Jumatatu zilijibidiisha kusafisha abiria wake mikono kabla kuingia kwenye basi, katika kile kilionekana kama kudumisha kiwango cha usafi.

“Mahali tumefikia janga hili la COVID-19 si la kutania tena, usalama lazima uanze na sisi wenyewe kama raia,” akasema mhudumu mmoja wa kampuni ya Virginia Coach ambayo mabasoinayohudumu Thika Superhighway.

Kampuni nyingine iliyoonekana kutilia mkazo mwelekeo uliotolewa ni ya Nicco.

Hata ingawa si wahudumu wengi waliokumbatia hatua hiyo, waliowajibika walijihami kwa sabuni maalum na kujituma kujali maslahi ya wateja wao na ya wao wenyewe. Aidha, kiasi kikubwa cha wasafiri walipiga foleni kwa matatu zilizotekeleza ushauri huo.

Akithibitisha visa viwili zaidi vya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini, Rais Uhuru Kenyatta Jumapili alihimiza umma kudumisha kiwango cha usafi. Kufikia sasa idadi ya walioambukizwa virusi hivyo imefikia watu watatu.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia mnamo Jumatatu pia alionya kuwa kampuni ambazo zitakiuka kanuni zilizowekwa katika mchakato mzima wa kudhibiti usambaaji wa COVID-19, leseni zao zitafutwa.