Habari

COVID-19: Kenya yaripoti visa 16 zaidi idadi jumla ikifika 336

April 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na NASIBO KABALE

WIZARA ya Afya Ijumaa imetangaza visa 16 vya maambukizi ya Covid-19 ambavyo vimeripotiwa nchini Kenya katika kipindi cha saa 24 zilizopita na kufannya idadi jumla ya visa vilivyoripotiwa kufika 336.

Waziri Msaidizi katika wizara Dkt Rashid Aman, akihutubia wanahabari amesema wagonjwa wa hivi punde ni sehemu ya idadi ya watu 946 ambao sampuli zao zilichukuliwa na kufanyiwa vipimo katika kaunti 12 katika kipindi hicho.

Amesema timu ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo hatari unaosababishwa na virusi vya corona imepata visa 11 katika Kaunti ya Nairobi na vitano katika Kaunti ya Mombasa.

Jijini Nairobi, visa vitano ni vya eneo la Dandora, viwili viwili katika maeneo ya City Park na Parklands huku maeneo ya Eastleigh na Pipeline yakiwa na kisa kimoja kila eneo.

Katika kaunti ya Mombasa maeneo ya Kiembeni, Centi Kumi, Stadium, Msikiti Nuru na Mulaloni yamekuwa na kisa kimoja kimoja.

“Tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kiripotiwe nchini Kenya mnamo Machi 13, 2020, vipimo 16,738 vimefanywa kiukamilifu,” amesema Dkt Aman.