COVID-19: Mbunge ataka ikiwezekana shule zifunguliwe Januari 2021
Na LAWRENCE ONGARO
KUTOKANA na jinsi hali ilivyo ya maradhi ya Covid-19, serikali isiwe na haraka ya kufungua shule hivi karibuni, amependekeza mbunge.
Kulingana na mbunge wa Thika Bw Patrick ‘ Jungle’ Wainaina, serikali inastahili kutathmini jinsi mambo yalivyo halafu ifikirie kufungua shule ifikapo Januari 2021.
“Janga la Covid-19 haliishi hivi karibuni na kwa hivyo ni vyema kujipanga zaidi. Mpango huo unahitaji washika dau wa elimu kujitokeza na mbinu tofauti jinsi wanafunzi wanavyostahili kurejelea masomo ya darasani katika shule kote nchini,” alisema Bw Wainaina.
Alisema huu ni wakati wa kuweka mikakati maalum katika shule zote ili kuwa tayari kwa kurejea kwa shughuli za kawaida.
“Jambo la muhimu kwa wakati huu ni kuona ya kwamba kuna maji ya kutosha katika kila shule. Barakoa zinastahili kupelekwa shuleni ili kila mwanafunzi avalie na kuwa salama; halafu kuwe na hamasisho kwa wanafunzi wote kupitia kwa walimu,” alisema mbunge huyo.
Alitoa mfano wa Thika akisema shule zaidi ya 20 za msingi zimepata matangi ya maji ya lita 10,000 kwa wakati mmoja.
Aliyasema haya mjini Thika alipokutana na wakazi wachache wa Thika ili kuwahamasisha kuhusu Covid -19.
Alisema walimu watakuwa kiungo muhimu kuona ya kwamba wanafuatilia mienendo ya wanafunzi hasa wale walioko kwenye shule za mabweni.
Kuhusu waumini kurejea maabadini, alipendekeza watu wazima pekee ndio wanastahili kwenda maombi kutoka saa tatu za asubuhi hadi saa saba za mchana upande wa Wakristo.
“Lakini watoto wanastahili kubaki nyumbani kabla mambo yawe kawaida. Janga la Covid-19 linastahili kushughulikiwa kwa umakini zaidi,” alisema Bw Wainaina.
Alisema kwa wakati huu cha muhimu zaidi ni kuona ya kwamba kila mtu ni lazima ajichunge mwenyewe kwa sababu serikali haitakuwa kila mara ikifuatana na wananchi kuhusu corona.
Mfanyabiashara katika kikundi cha Jubilee Self-help Group Bi Julia Kiongo, anapinga pendekezo la wanafunzi kurudi shuleni Septemba.
“Mimi kama mzazi singetaka mtoto wangu kurejea shuleni wakati huu bila kuwa na mikakati maalum iliyowekwa,” alisema Bi Kiongo.
Alisema hamasisho kwa wanafunzi ni muhimu kwanza kwa sababu iwapo mwanafunzi ataambukizwa virusi vya corona, italazimisha shule nzima kufungwa mara moja.
Kulingana na ripoti ya serikali kuhusu hali ya Covid-19, kuna visa vya zaidi ya watu 5,000 ambapo waliopona ni 1,900 lakini watu wapatao 137 wamefariki nchini.