Habari

COVID-19: Visa 152 vipya, 57 wapona na 4 wafariki

June 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

WATU 152 wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona nchini Kenya ndani ya muda wa saa 24 zilizopita na kufikisha 3,457 idadi jumla ya maambukizi kufikia Jumamosi.

Visa hivyo viligunduliwa baada ya sampuli 3,403 kupimwa kati ya Ijumaa na Jumamosi, na hivyo kufikisha 112,171 idadi ya sampuli ambazo zimepimwa nchini tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipogunduliwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Wagonjwa hawa wapya wote ni Wakenya ambapo 116 ni wanaume na 36 ni wa jinsia ya kike.

Akitoa takwimu hizo Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman ameongeza kuwa jumla ya wagonjwa 57 wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Hii ina maana kuwa kufikia sasa (Jumamosi) jumla ya wagonjwa 1,221 wamepata afueni ishara kwamba wahudumu wetu wa afya wanafanya kazi nzuri,” Dkt Aman amesema kwenye kikao na wanahabari nje ya jumba la Afya, Nairobi.

Hata hivyo, idadi ya wagonjwa ambao wamefariki kutokana na Covid-19 imegonga 100 baada ya wengine wanne kukata roho ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.

Kwa mara nyingine Nairobi ingali inashikilia nafasi ya kwanza kwa kuandikisha maambukizi mapya 70 miongoni mwa 152 yaliyothibitishwa Jumamosi. Mombasa inafuata kwa visa (14), Busia (16), Kiambu (9), Machakos na Migori visa vitatu kila moja na Kisumu (2).

Kaunti za Taita Taveta, Nakuru, Narok na Uasin Gishu zimethibitisha kisa kimoja, kila moja.

Visa vya maambukizi katika kaunti ya Mombasa vinapatikana katika maeneo bunge yafuatayo; Nyali (14), Mvita (10), Likoni (7), Kisauni (6) na Changamwe (4).

Na visa vyote 16 vilivyothibitishwa katika kaunti ya Busia ni madereva wa matrela katika kituo cha mpakani cha mji wa Malaba.

Dkt Aman amekariri kuwa ipo haja ya kuwepo kwa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya maeneo ya mijini na yale ya mashambani katika vita dhidi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

“Hii ni kutokana na hali kwamba watu wengi wanasafiri kutoka mijini hadi mashambani,” akaeleza

Akaongeza: “Maambukizi ya Covid-19 miongoni mwa madereva yanaendelea kuongezeka kwa sababu ya kutozingatia mikakati na sheria tulizoweka.”

Amehimiza madereva na wamiliki wa malori kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kuingia barabarani.

Katika maeneo ya mipakani, amesisitiza kuwa madereva walio cha cheti cha Covid-19 ndio pekee wataruhusiwa kuingia nchini.

Dkt Aman amesema ni sharti wahakikishe stakabadhi hiyo inawasilishwa saa 48 kabla ya kuanza safari.

Kikao cha kesho Jumapili kitaandaliwa Othaya, Nyeri na cha Jumatatu Olkalou, Nyandarua.