Habari

COVID-19: Visa jumla nchini Kenya vyafika 1,745

May 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

MAGDALENE WANJA na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya Ijumaa imetangaza visa 127 vipya vya Covid-19 baada ya sampuli 3,831 kufanyiwa vipimo kipindi cha saa 24 zilizopita huku visa jumla nchini Kenya vikifika 1,745 sasa.

Kaunti za Nairobi na Mombasa bado zinaongoza kwa idadi ya maambukizi.

Akitangaza idadi hiyo ya maambukizi mapya, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Mercy Mwangangi amesema kuwa katika kaunti ya Nairobi, mtaa wa Kibera unaongoza ukiwa na visa 49.

“Katika muda huo wa kipindi cha saa 24, watu 17 wamekubaliwa kuondoka hospitalini baada ya kupona lakini tunasikitika watu wanne kutoka Mombasa wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo,” amesema Dkt Mwangangi.

Waliopona sasa ni 438 nayo idadi ya waliofariki nchini kutokana na Covid-19 nchini sasa ni 62.

Amefurahishwa na Wakenya akisema idadi ya watu wanaojitokeza kupimwa inaendelea kuongezeka, lakini pia akasikitika kwamba baadhi ya watu wanatumia njia za mkato kuingia Nairobi na Mombasa, miji ambayo amri ya kuingia na kutoingia hadi Juni 6, 2020, inaendelea kutekelezwa.

Dkt Mwangangi ameonya kuwa watakaopatikana wakikiuka amri hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.

“Kutoroka miji ambayo shughuli za kuingia na kutoka zimesitishwa ni kuhamisha virusi hadi maeneo mengine,” amesema.

Kaunti zinazoathiriwa na zuio la ama kuingia au kutoka ni Nairobi, Kilifi, Kwale na Mombasa na hali imekuwa hivyo kuanzia Machi 27, 2020.

Hata hivyo, visa vya watu kuingia na kutoka maeneo yaliyoathirika vinaendelea kuripotiwa.

“Wakenya wajue hali ingali tete. Tunasihi watu wajitokeze kupimwa Covid-19 na ikiwa ungali salama, usidhani huwezi ukaambukizwa; jihadhari kwa kuzingatia mikakati iliyowekwa,” Dkt Mwangangi akaeleza.

Idadi ya kaunti ambazo zimeripoti visa vya corona kufikia sasa ni 32 kati ya kaunti 47.