COVID-19: Visa jumla vyafika 6,070
Na BERNARDINE MUTANU
IDADI ya visa vipya vya Covid-19 imeanza kupanda kwa kasi kwa sababu ya maambukizi kuongezeka katika jamii na vilevile uwezo wa kupima sampuli nyingi kutoka kwa watu nchini.
Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Mercy Mwangangi amesikitika Jumapili kwamba hali inazidi kuwa mbaya nchini kote akiwahimiza raia kufuata na kuzingatia sheria na kanuni zilizotolewa kudhibiti kuenea kwa Covid-19.
“Wakenya wanafaa kuchukua hatua bila kungoja serikali na maafisa kuwashinikiza kufuata taratibu za kuepuka maambukizi ya Covid-19,” amesema Dkt Mwangangi akihutubu jijini Nairobi.
Aidha, katika muda wa saa 24 zilizopita, Dkt Mwangangi amesema watu 259 wamepatikana na virusi vya corona baada ya wataalamu kuchukua sampuli 2,718 na kuzifanyia vipimo.
Idadi hii sasa inafanya visa jumla kuwa 6,070
Katika visa vya hivi punde, wagonjwa 159 ni wanaume nao 100 ni wa jinsia ya kike.
Wagonjwa watatu ni raia wa kigeni.
Nairobi ingali inaongoza kwa visa vipya leo Jumapili ikirekodi 127 nayo Kaunti ya Lamu ndiyo ya hivi punde kuwa na wagonjwa wa Covid-19 na hivyo kupandisha idadi ya kaunti zilizo na wagonjwa kufika 41 kati ya zote 47 nchini.
Wagonjwa wawili zaidi wameangamia wakifikisha watu 144 idadi jumla ya vifo kutokana na maradhi haya nchini.
Serikali za kaunti zimehimizwa zihakikishe zinaimarisha mchakato wa kupima sampuli kuweza kutambua wagonjwa, kuimarisha mbinu za kutafuta watu waliotangamana na wagonjwa na vilevile ziwe tayari kuwapokea Wakenya, lakini pia wakazi wengine wanaoweza kuhitaji matibabu.