Habari

COVID-19: Visa vya maambukizi nchini vyasalia saba

March 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya nchini Kenya imesema matokeo ya vipimo vinane kipindi cha saa 24 zilizopita yameonyesha hakuna kisa chochote kipya cha maambukizi nchini na hivyo kumaanisha idadi ya walio na Covid-19 inasalia watu saba.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, waziri Mutahi Kagwe amesema kufikia Alhamisi, watu hao wanane ambao sampuli zao zilichukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo kipindi hicho sasa wanafanyiwa mchakato waruhusiwe kuondoka hospitalini.

Kufikia sasa Kenya imepima visa 173.

“Leo (Alhamisi) hatujaripoti kisa chochote cha Covid-19,” amesema waziri akisisitiza visa vyote vya kushukiwa ni sharti maafisa wavifanyie vipimo.

Amesema watu saba ni Wakenya huku yule wa nane akiwa ni raia wa Burundi, lakini wote wakiwa ni waliokuwa wametoka nje ya nchi.

“Wakenya wote saba wanaendelea vizuri kiafya,” amesema.

Amesema pia kwamba zaidi ya watu 600, 000 waliongia nchini Kenya tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kiripotiwe wamekaguliwa.

Serikali inaendelea kuhimiza umma kudumisha kiwango cha usafi, ikiwa ni pamoja na kutilia mkazo utaratibu uliotolewa ili kudhibiti maenezi zaidi ya virusi hivyo.

Mapema wiki hii Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kufungwa kwa shule na taasisi zote za elimu ya juu nchini.

Waziri Kagwe amesema aagizo la Rais halimaanishi wazazi wawatume watoto wao kwenye masoko au maeneo ya kupumzika, kujiburudisha na kutangamana na wenzao ovyo ila linalenga kuzuia maambukizi zaidi ya Covid – 19 hasa katika mikutano ya watu.

“Huu si wakati wa holidei, ni wakati wa kupambana na Covid-19. Tuliposema shule zifungwe, hatukumaanisha watoto watumwe masokoni au wapelekwe maeneo ya kupumzika, kujiburudisha na kutangana na wenzao. Tulipania kuondoa mtangamano huo,” Bw Kagwe amesema.

Waziri huyo pia ametangaza kwamba kuanzia Jumamosi, Machi 21, idara ya afya kwa ushirikiano na shirika la msalaba mwekundu na maafisa wa usalama, itaanza kupima watu maeneo yanayoshukiwa kuwa na uwezekano wa maambukizi ya Covid-19.

Pia ameamuru mfumo wa Nyumba 10 kupitia machifu na manaibu wao kusaidia katika zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kutambua kila mkazi na kutathmini hali yake kiafya.

Ameyataka maeneo ya burudani kufuata kanuni zilizotangazwa, kama vile kuhifadhi kiwango cha hadhi ya juu cha usafi pamoja na kuendesha shughuli zao muda uliowekwa, la sivyo leseni zao zifutiliwe mbali.

Aidha, waziri ameeleza kushangazwa kwake na ‘habari’ zinazoenezwa mitandaoni kuwa jiji la Nairobi litafungwa kwa hofu ya Covid-19, watu wafurushwe na wanajeshi wapige doria, akitaja habari hizo kama za uongo mtupu na zinazopotosha umma.

Ameonya kuwa yeyote atakayepatikana akisambaza habari za aina hiyo atakamatwa, akabiliwe vikali kisheria, “na tutampeleka katika Hospitali ya Mbagathi ajionee hali ilivyo aripoti kutoka humo”.

“Ninasihi Wakenya wawe watulivu, habari za mitandao ni potovu na zinazozua taharuki,” akasema.

Hata hivyo, Waziri Kagwe ametaka umma kujua kuwa virusi vya corona ni hatari, akihimiza watu wachukue tahadhari ya kujizuia kuambukizwa.

Unahimizwa kudumisha kiwango cha usafi wewe mwenyewe na katika mazingira yako, hasa kwa kunawa mikono kwa jeli.

Pia unatakiwa kuepuka mikutano ya hadhara na unapotangamana na watu hakikisha umesimama au kuketi angalau mita moja kutoka kwa uliye karibu naye.

Kwa wanaoweza kufanyia kazi zao nyumbani, wanahimizwa kufanya hivyo.