COVID-19: Wizara yazitaka serikali za kaunti zijali maslahi ya CHWs
Na SAMMY WAWERU
WIZARA ya Afya imesema suala la kuwapa malipo wahudumu wa afya wa kijamii – CHWs – wanaojitolea kushughulikia wagonjwa wa Covid-19 wanaotunziwa nyumbani ni jukumu la serikali za kaunti.
Waziri Msaidizi katika Wizara, Dkt Rashid Aman amesema serikali za kaunti zinapaswa kuwa na mpango maalum kushirikisha wahudumu hao katika malipo.
Huduma za wahudumu hao zilizinduliwa miezi kadhaa iliyopita ili kusaidia kuondoa msongamano wa wagonjwa wa Covid-19 katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
Aidha, mpango wa kutumia wahudumu wa afya wa kijamii wa kujitolea, unalenga wagonjwa wasioonyesha dalili za Covid-19, Wizara ya Afya ikiusifia kutokana na idadi ya juu ya wagonjwa waliopona kuupitia.
Waziri Aman amesema Alhamisi ikiwezekana serikali husika za kaunti ziafikiane namna ya kulipa wahudumu hao, akiwapongeza kwa kusaidia pakubwa katika vita dhidi ya janga la corona nchini.
“Ili kusaidia kupambana na ugonjwa huu, tumekumbatia mpango wa wahudumu wa afya wa kijamii wa kujitolea. Ni jukumu la kaunti kuwaajiri. Ikiwezekana, wawe na mpango na kukubaliana nao namna ya kuwalipa,” Dkt Aman akasema akijibu swali lililoibuliwa na wanahabari wakati akitoa taarifa jijini Nairobi.
Baadhi yao, wamekuwa wakijigharimia kusafiri ili kuhudumia wagonjwa katika makazi yao, pamoja na mahitaji mengine muhimu kufanikisha mpango huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini, Dkt Patrick Amoth amesema kuna zaidi ya wahudumu 90,000 wa afya wa kijamii wa wanaojitolea katika kaunti mbalimbali nchini.
“Zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaothibitishwa kupona, wanatunziwa nyumbani,” Dkt Amoth amedokeza.
Kufuatia mpango huo unaosifiwa kupunguza gharama ya matibabu kwa wagonjwa, afisa huyo amekiri kuwa idadi ya wagonjwa wanaotunziwa katika vituo vya afya inaendelea kushuka.
Amesema zaidi ya asilimia 93 ya wagonjwa waliopatikana na Covid-19, hawaonyeshi dalili za maambukizi.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha visa 373 vipya vya Covid-19, idadi hiyo ikifikisha jumla ya visa 33,389 vya corona vilivyothibitishwa tangu kutangazwa kwa kisa cha kwanza Machi 13, 2020.
Hivi 373 vinatokana na sampuli 4,663 zilizochukuliwa na kufanyiwa vipimo.