Habari

Covid-19 yaumiza matapeli

April 25th, 2020 2 min read

WANDERI KAMAU na VALENTINE OBARA

MIPANGO inayoendelezwa na serikali kupambana na virusi vya corona, imekuwa pigo kwa matapeli ambao wangependa kutumia janga hilo kujinufaisha kibinafsi.

Hii ni baada ya serikali kuamua kubadili mitindo yake ya kushughulikia majanga katika vita dhidi ya corona, hatua ambayo imewanyima matapeli nafasi ya kuunda pesa.

Masuala ambayo yalikuwa hatarini kuvurugwa na tamaa ya watu wachache wasiojali umma ni kama vile ununuzi wa vifaa vya matibabu, ununuzi na usambazai wa mahitaji ya kila siku ya wananchi waliolemewa ikiwemo misaada ya kifedha.

Kwa jumla, serikali imepanga kutumia Sh40 bilioni kwa mahitaji ya kupambana na virusi hivyo.

Matamshi ya viongozi wakuu serikalini yamefichua wazi kwamba mikakati inayochukuliwa ni kwa kusudi la kuzima wafanyabiashara waliokuwa wakisubiri kunyakua kandarasi mbalimbali kisha kudai fedha nyingi kupita kiasi kutoka kwa serikali.

Ijumaa, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, alifichua kwamba baadhi ya matapeli walikuwa wakiuza vazi moja la kulinda wahudumu wa afya kutokana na maambukizi ya viini kwa Sh15,000.

Hili ni kinyume na sasa ambapo vazi moja lililotengenezewa humu nchini linauzwa kwa bei ya wastani ya Sh4,500.

Kulingana na Bw Kagwe, matapeli hao sasa wameanza kujaribu kushawishi wakuu serikalini kwamba vifaa vinavyotengenezwa na viwanda vya humu nchini havina ubora unaohitajika.

“Baadhi ya wafanyabiashara hao walikuwa wakitumia hila kufaidika kwa kutuuzia vifaa hivyo kwa bei ya juu. Washonaji wetu wa humu nchini wanafanya kazi nzuri ifaavyo,” akasema Bw Kagwe.

Alisema daktari huhitajika kubadilisha magwanda yake ya kimatibabu kila wakati anapohudumia mgonjwa tofauti, na hivyo basi kutumia Sh15,000 kila wakati ni utapeli wa hali ya juu.

Vyuo vikuu, taasisi za elimu ya juu na viwanda mbalimbali vimeibuka kutengeneza mavazi na vifaa vinavyotakikana kwa dharura katika vita dhidi ya corona.

Kando na mavazi ya madaktari, vitu vingine vinavyoundwa ni maski zinazotumiwa na umma, dawa za kuua viini vya corona, sanitaiza, vifaa vya kusaidia wagonjwa kupumua miongoni mwa vingine.

Taasisi hizo zinajumuisha Kiwanda cha Kutengeneza Nguo cha Kitui (Kicotec), Rivatex, Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Chuo Kikuu cha Kenyatta, na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa.

“Mafundi wetu wanafanya kazi ya kuridhisha. Tunaamini kuwa katika siku kadha zijazo, suala la kupata maski halitakuwa lenye utata hata kidogo kwa mwananchi,” akasema Bw Kagwe.

Kwa upande mwingine, ununuzi na usambazaji wa mahitaji ya umma ulikabidhiwa kwa kamati inayosimamiwa na wakuu wa mashirika ya kibinafsi.

Rais Uhuru Kenyatta aliunda kamati hiyo inayosimamiwa na Bi Jane Karuku kama njia mojawapo ya kufanikisha uwazi na uadilifu katika shughuli ya matumizi ya fedha na bidhaa zinazotoka kwa wahisani.

Alipotangaza kuongeza serikali za kaunti fedha, Rais Kenyatta alisisitiza ni sharti wanunue vifaa vinavyotengenezwa humu nchini ili kuzuia ufujaji wa fedha za umma. Kwa kufanya hivyo, alizima uwezekano wa wafanyibiashara walio na ushawishi serikalini kutumia uwezo walio nao kuuzia serikali bidhaa kama vile vyakula kwa bei ghali kupita kiasi.

Vilevile, hatua ya serikali kuu kutuma pesa moja kwa moja kwa Wakenya wenye mahitaji kupitia simu pia imesaidia kuepusha pesa hizo kuibwa.

Vilevile, mwelekeo huo umezuia hitaji la kuagiza vyakula vya msaada kutoka nchi za nje, hali ambayo ingetoa mwanya kwa matapeli kuingilia kati ili wapate zabuni kwa njia za mkato.