Habari

Deni la Kenya laongezeka kwa Sh1 trilioni serikali ikiendelea kukopa bila breki

Na PETER MBURU October 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DENI la umma nchini Kenya liliongezeka kwa zaidi ya Sh 1 trilioni kati ya Januari na Agosti 2025, na kufikia jumla ya Sh11.9 trilioni, hatua inayoongeza mzigo kwa walipa ushuru huku serikali ikiendelea kukopa zaidi kutoka soko la ndani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Fedha, Sh697.4 bilioni za ongezeko hilo zilitokana na mikopo ya ndani, huku mikopo ya nje ikiongeza Sh346.3 bilioni. Hii inaashiria mwelekeo mpya wa serikali kupendelea mikopo ya ndani kutokana na riba nafuu.

Kwa sasa, mikopo ya ndani inachangia asilimia 54.9 ya jumla ya deni, huku mikopo ya nje ikichangia asilimia 45.1. Waziri wa Fedha, John Mbadi, alisema serikali iliepuka kukopa nje kutokana na athari za kushuka kwa thamani ya shilingi, ambayo ilifikia kiwango cha juu cha Sh 165 kwa dola moja ya Amerika na kuongeza deni la nje kwa Sh1 trilioni bila hata kuchukua mkopo mpya.

Mbadi alieleza kuwa serikali itarudia mikopo ya nje endapo itapata masharti nafuu kutoka kwa taasisi za kimataifa. Deni la taifa pia lilipanda zaidi ya trilioni moja mwaka wa 2023, na mara ya kwanza ilikuwa 2020 wakati wa janga la Covid-19.

Katika kipindi cha miezi minne hadi Agosti 2025, serikali ilikopa mikopo minne yenye thamani ya Sh95.5 bilioni, ikiwemo mkopo wa Sh16.4 bilioni kutoka Hazina ya Kimataifa ya Maendeleo ya Kilimo kusaidia kilimo na mazingira, hasa kwa makundi yaliyo hatarini kama wanawake na vijana.