Habari

Dhamana ya Sh500,000 kila mmoja kwa kuiba Biblia 500

May 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

WANAUME watatu walishtakiwa Jumatatu kwa wizi wa Bibilia 500. Reuben Rogoi Maina, John Mapesa Andulu na Josephat Gatheru (pichani) walikanusha mashtaka mawili ya wizi wa Biblia kutoka kituo cha utafsiri wa Bibilia- Bible Translation and Literacy (EA) mtaani Upperhill, Nairobi.

Shtaka dhidi Maina na Andulu lilisema kuwa mnamo Mei 16, 2019 wakiwa na nia ya kulaghai walipokea Biblia 300 za News King James version na nyingine 200 za Good News International Version wakidai hundi ya Sh920,000 waliyompa Bi Faith Mawia Mulunga ilikuwa halisi.

Hundi hiyo nambari 000076 ya Sh920,000 ilikuwa ilipwe na Benki ya Cooperative tawi la Masai Mall.

Bw Andulu na Bw Gatheru walikabiliwa na shtaka peke yao kuwa mnamo Mei 16 walikutwa na gari la nambari ya usajili KCH 596 muundo wa Toyota Fielder lenye rangi nyekundu likisafirisha Biblia hizo zenye thamani ya Sh680,000.

Washukiwa walikanusha mashtaka dhidi yao na kuomba waachiliwe kwa dhamana. Ombi hilo halikupingwa na kiongozi wa mashtaka.

Kila mmoja aliamriwa awasilishe dhamana ya Sh500,000. Hakimu mkuu Francis Andayi aliamuru upande wa mashtaka uwakabidhi washtakiwa hao nakala za mashahidi waandae ushahidi wao.

Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili upande wa mashtaka ueleze ikiwa umewakabidhi washukukiwa hao nakala za ushahidi.