Dida amtaka Uhuru aheshimu Raila
Na LEONARD ONYANGO
ALIYEKUWA mwaniaji wa urais Abduba Dida amemrai Rais Uhuru Kenyatta amheshimu kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga kwa uzoefu wake kisiasa, na akubali kufanya mazungumzo naye.
Bw Dida aliyekuwa akizungumza wakati wa mahojiano na runinga moja humu nchini Jumatatu asubuhi alisema: “Rais anafaa kumheshimu Raila na kusikiliza maoni yake. Raila amejizolea tajriba katika siasa hivyo hafai kupuuzwa,” akasema kiongozi wa chama cha Alliance for Real Change.
Bw Dida ambaye amewania urais mara mbili bila mafanikio, hata hivyo, alimshukuru Rais Kenyatta kwa kutotumia polisi kusambaratisha ya kumwapisha Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’.
“Kuapishwa si vibaya, hata mimi naweza kujiapisha kesho almradi niwe na watu kumi wanaoniamini,” akasema Bw Dida.
Aibiwa simu jijini
Kwenye mahojiano hayo, Bw Dida ilifichua kuwa aliibiwa kioo cha gari lake katikati mwa Jiji la Nairobi. Kwa sasa, anawataka Wakenya kuwa waaminifu na kumcha Mungu baada ya kupoteza simu na kioo cha gari lake.
Bw Dida alisema vijana walimpokonya simu yake alipokuwa akiitumia karibu na shule ya Upili ya Moi Forces katika eneobunge la Kamukunji, Nairobi.
“Kila Mkenya anastahili kuwa mwaminifu kwani kila mtu ni kiongozi katika familia yake, jamii au nchini. Jana nilipokuwa nimeegesha gari langu katikati mwa jiji wakora waliniibia kioo na baadaye wakanipokonya simu karibu na shule ya upili ya Moi Forces,” akasema Bw Dida.