DONDOO: Lofa azusha mazishini Kitui akidai ndiye mume halisi wa marehemu
KIOJA kilizuka katika mazishi yaliyofanyika eneo la Tsikuru mjini Kitui baada ya lofa kudai kuwa ndiye mume halisi wa marehemu.
Polo alidai kwamba ndiye alikuwa mwanamume wa kwanza kumuoa marehemu kabla ya wao kuachana.
Inasemekana polo aliinuka na kuomba nafasi ya kusema jambo na wengi wakafikiri huenda alikuwa na deni la marehemu na alitaka kuweka wazi.
“Aliyelazwa hapa alikuwa mke wangu, nilikuwa nampenda sana. Hadi leo katika kifo chake ningali nampenda. Mimi ndiye mumewe halali. Hata mahari nililipa,” lofa aliambia waombolezaji.
Madai ya lofa yalishangaza wengi ikizingatiwa kwamba alikuwa ameachana na marehemu kwa miaka mingi tu na akaolewa na mwanamume mwingine.