WATEJA katika baa moja mtaani Mwiki, Kasarani, jijini Nairobi walishangaa burudani ilipokatizwa ghafla wakati pasta aliingia kilabuni na kumfurusha msanii aliyekuwa akiwatumbuiza kwa kuwachezea kinanda cha piano.
Msanii huyo huwa mwalimu wa kwaya kanisani mwa pasta na huruhusiwa kwenda nyumbani na baadhi ya ala za muziki za kanisa ili akafanye mazoezi wakati wake.
Siku ya kisa pasta akiwa katika pilkapilka zake aliona tangazo lililomuonyesha mwalimu wao wa kwaya kwamba angekuwa akitumbuiza wateja katika kilabu moja maarufu.
Mchungaji akafanya uchunguzi wake akihofia kuwa labda polo hutumia vyombo vya kanisa vibaya.
Akasubiri hadi usiku pale msanii alianza kutumbuiza wateja kilabuni akaingia kujionea ukweli wa mambo. Ni hapo alipomnasa akitumia piano ya kanisa.
“Toka hapa mara moja!” pasta alimfokea jamaa na kumfurusha nje.