Sonko akamatwa mjini Voi mara baada ya agizo la DPP
Na SAM KIPLAGAT
GAVANA wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko amematwa mjini Voi mara baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kutoa agizo atiwe mbaroni mapema Ijumaa.
Sonko anayehusishwa na ufisadi atashtakiwa kuhusu kupotea kwa Sh357 milioni.
DPP amesema ushahidi upo wa kutosha.
Sonko na wengine kadhaa katika serikali ya kaunti wanatarajiwa kushtakiwa kuhusiana na kupotea kwa Sh357 milioni.
DPP Noordin Haji hata hivyo amesikitika kwamba baadhi ya asasi na watu wenye nyadhifa wanahujumu vita dhidi ya mazoea ya ukwepaji uwajibikaji wa kisheria.
“Baadhi ya asasi hutuzima kutoa agizo la kuwakamata baadhi ya watu,” amesikitika Bw Haji mnamo Ijumaa asubuhi jijini Nairobi.
Wakuu wengine wanaowindwa ni katibu wa kaunti Peter Mbugua, wanachama wa kamati ya tenda Patrick Mwangangi, Samuel Ndung’u, Edwin Kariuki, Lawrence Mwangi, Preston Miriti miongoni mwa wengine.
Gavana Sonko na hao wengine watakabiliwa na mashtaka ya kupanga kutekeleza uhalifu wa kiuchumi, kukosa kufuata sheria kwa kukusudia na vilevile mgongano wa kimaslahi.
Bw Haji amesema uchunguzi na upelelezi uliofanywa na Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) umesaidia kupatikana kwa ushahidi wa kutosha kumfungulia Sonko mashtaka.