Habari

Duale ataka viongozi wa Kiislamu kuunga sheria ya kudhibiti mitandao nchini

Na CECIL ODONGO October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Afya Aden Duale amewataka viongozi wa Kiislamu kuunga mkono sheria mpya ya uhalifu wa mtandaoni, akisema inalenga kulinda maadili ya jamii, hasa watoto dhidi ya maudhui machafu yanayosambazwa mitandaoni.

Akizungumza Alhamisi katika Msikiti wa Jamia, Nairobi, wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachoelezea historia ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka 100, Bw Duale alisema ni wajibu wa viongozi wa dini na wanasiasa “kutetea lililo sahihi” na kulinda maadili ya vijana.

“Kifungu cha 27 cha Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni kilipitishwa wakati nilikuwa Kiongozi wa Wengi Bungeni. Kifungu hiki hulinda watoto wetu dhidi ya maudhui ya ngono na mambo mengine yanayopotosha maadili. Mahakama ilitangaza kuwa kifungu hicho ni halali miaka miwili iliyopita, lakini juzi nikashangaa kuona jaji mwingine akikitaja kuwa kinyume cha Katiba,” alisema Bw Duale.

Aliongeza kuwa viongozi hawapaswi kuogopa kutetea misingi ya maadili.

“Viongozi wa dini na wanasiasa wasisite kuunga mkono sheria hii ili kuokoa watoto wetu. Tusijifanye waoga wakati tunajua tunalotetea ni sahihi,” alisema.

Mnamo Oktoba 23, Mahakama Kuu jijini Nairobi ilisimamisha utekelezaji wa vifungu vya 27(1)(b)(c) na (2) vya sheria hiyo, vilivyokuwa vikipinga usambazaji wa mawasiliano ya kimakusudi yanayoweza kudhuru sifa, faragha au afya ya akili ya mtu mwingine.

Hatua hiyo ilifuatia ombi lililowasilishwa na mwimbaji wa injili Reuben Kigame na Tume ya Haki za Binadamu (KHRC), waliodai vifungu hivyo vinaingilia uhuru wa kujieleza mtandaoni.

Mwenyekiti wa Msikiti wa Jamia Osman Warfa akihutubu wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachozungumzia miaka 100 ya uwepo wa msikiti huo. PICHA| Boniface Bogita

Rais William Ruto alitia saini marekebisho ya sheria hiyo kuwa sheria kamili wiki moja kabla ya uamuzi huo wa mahakama.

Bw Duale alisema maudhui hatari mtandaoni yamechangia ongezeko la visa vya msongo wa mawazo na kujiua miongoni mwa vijana.

“Vijana wengi wako mitandaoni. Hilo si tatizo, lakini wanafanya nini huko? Maimamu na viongozi wa taasisi za Kiislamu lazima waongoze kwa kuwashauri vijana wetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa Msikiti wa Jamia, ulioko katikati ya jiji la Nairobi, una jukumu la kuonyesha uongozi wa mfano kwa wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini.

Akihutubu wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Mskiti wa Jamia Sheikh Osman Warfa, alisema uongozi wa msikiti huo unajivunia hatua ambayo imepigwa kwa miaka 100 ya uwepo wake.

“Msikiti huu umeshiriki miradi mbalimbali ya kuinua jamii na msingi ambao uliwekwa na walioujenga umedumu hadi leo. Umetoa nafasi ya ajira kwa wengi na ndio unazingatiwa kuwa mama ya misikiti mingine kote nchini,” akasema Sheikh Warfa.