Habari

Eastleigh yaamka tena kibiashara baada ya majuma kadhaa ya kimya

June 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MTAA wa Eastleigh, Nairobi, Jumapili ulirejelea hali yake ya kawaida huku wenye biashara wakifungua saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusitisha amri ya kutoingia na kutotoka eneo hilo.

Kulingana na data kutoka idara za serikali biashara ya thamani ya takriban Sh200 milioni huendeshwa katika eneo hilo kila siku.

Katika barabara ya Eastleigh First Avenue, malori kadha yalionekana, bidhaa zikipakuliwa kutoka kwa magari hayo huku wahudumu wa matatu na waendeshaji wa bodaboda wakirejelea hudumu za kuwasafirisha watu.

Vizuizi vya barabarani ambavyo vimedumu katika njia za kuingia na kuondoka mtaani humu kwa siku 30 zilizopita havikuwepo Jumapili.

Kelele zilirejelea katika barabara nyingi za mtaa huo wa kibiashara huku wachuuzi wakitumia mbinu mbalimbali kuwavutia wateja.

Misongamano ya watu na magari ilirejelea tena katika barabara kadhaa huku majumba makubwa ya kibiashara kama vile Garissa Lodge, Hongkong na Bankok yakirejelea shughuli za kawaida.

“Sasa tunaweza kuwatafutia watoto wetu chakula kwani tumefungua biashara zetu,” mama mmoja akasema.

Eastleigh na Old Town Mombasa ni maeneo yaliyofungwa mwezi mmoja uliopita baada ya kuandikisha idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hiyo iliathiri uchumi wa Eastleigh; eneo ambalo ni la pili kwa ukubwa kibiashara Nairobi nyuma ya Westlands.

Takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa Eastleigh huchangia asilimia 25 ya jumla ya mapato ya Kaunti ya Nairobi.

“Mchango wa Eastleigh katika uchumi wa Nairobi na taifa kwa ujumla hauwezi kudunishwa,” anasema mkazi mmoja ambaye ni mfanyabishara eneo hilo.

Kando na kuchangamkia kufunguliwa tena kwa shughuli za kawaida katika eneo hilo, wakazi pia walielezea kuridhishwa kwa hatua ya serikali kuongeza muda wa kuanza kafyu kutoka saa moja hadi saa tatu usiku.

“Huu mpangilio mpya wa kafyu sasa utatuwezesha kuwa na wakati mwingi wa kufanya biashara na kuongezea mapato yetu,” akasema Meshack Maina ambaye ni mfanyabiashara eneo hilo.

Wafanyabiashara walisema walipata hasara kubwa zaidi wakati wa kipindi cha siku 30 ambapo mtaa huo ulifungwa huku wakiitaka serikali kutoa misaada kwa familia maskini.