Familia ya Kibaki yatoa ushahidi kortini kupinga ‘watoto wawili haramu
FAMILIA ya aliyekuwa Rais Mwai Kibaki imewasilisha ushahidi mahakamani ikipinga madai ya watu wawili wanaodai kuwa watoto wa marehemu wanaotaka warithi sehemu ya mali yake.
Katika kesi inayoendelea mbele ya Jaji Erick Ogolla, ilielezwa kuwa mwanawe Kibaki, James Mark Kibaki, aliwaajiri wachunguzi wa kibinafsi kuthibitisha iwapo Jacob Ocholla (miaka 67) na Bi JNL (miaka 64) kweli ni watoto wa Rais huyo wa zamani.
Wawili hao waliwasilisha kesi kortini wakisema walizaliwa baada ya mama zao kukutana na Kibaki miaka ya 1950 wakiwa masomoni Uganda na Uingereza.
Bi JNL aliungwa mkono na mama yake ambaye aliwasilisha hati ya kiapo akidai Kibaki ndiye baba wa mwanawe.
Hata hivyo, ripoti ya mpelelezi binafsi Sebastian Omboto wa kampuni ya Advanced Forensics Limited inasema hakuna ushahidi unaothibitisha madai hayo.
Kwa upande wa Bw Ocholla, Omboto alisema jina lake halisi ni George Jacob Ojuka Ocholla kutoka Ugunja, Kaunti ya Siaya. Ripoti inaonyesha kuwa yeye ni mtoto wa sita kati ya ndugu 11, na mmoja wa ndugu zake, James Umira, alikanusha madai kuwa Kibaki ni baba yao.
“Jacob anaonekana kuongeza jina ‘Mwai’ baada ya kifo cha Rais Kibaki ili kuonekana kana kwamba walikuwa na uhusiano wa damu,” alisema mpelelezi.
Aidha, Bw Umira alisema mama yao alikuwa mama wa nyumbani na hakuwa na nafasi wala mazingira ya kukutana na Kibaki na kisha kuficha siri hiyo kwa mumewe na familia.
Ushahidi wa Bw Ocholla kwamba alikutana na Kibaki katika Hoteli ya Mombasa Beach miaka ya 1980 pia ulipuuzwa na mfanyakazi wa zamani wa hoteli hiyo, Benjamin Bongo, aliyesema hakuwahi kuwaona pamoja na wafanyakazi hawakuruhusiwa kushirikiana kijamii na wateja.
Kuhusu Bi JNL, Omboto alisema mama yake aliandika wasifu wake bila kumtaja Kibaki na badala yake alimwelezea mume wake halali aliyemuoa kabla ya kuenda Uingereza.
Ripoti inaonyesha kuwa mama ya Bi JNL alienda Uingereza kwa masomo mwaka 1958 akiwa tayari na watoto wawili na akiwa ameolewa.
Familia ya Kibaki, ikiongozwa na binti yake Judith Wanjiku Kibaki, ilikana madai ya wote wawili, ikisema hawajawahi kushiriki nao hafla yoyote ya kifamilia wala kuwatambua kama ndugu.
“Kufanana kwa uso pekee, hata kama kupo, hakuthibitishi uhusiano wa damu,” alisema Bi Wanjiku kuhusu Bw Ocholla.
Bi Wanjiku pia alisema kwamba Kibaki hakuwahi kumtambua Bw Ocholla kuwa mwanawe, na hakuna ushahidi wa maandishi au ithibati kutoka kwa mtu mwingine kuhusu madai hayo.
Kesi hiyo itaendelea kusikizwa Mei 14, 2026 ambapo Bw Ocholla anatarajiwa kuulizwa maswali na mawakili kuhusu ushahidi wake.
Rais mstaafu Mwai Kibaki alifariki Aprili 22, 2022 akiwa na umri wa miaka 90 na alizikwa nyumbani kwake Othaya katika Kaunti ya Nyeri.