HabariSiasa

Ford Kenya kumtia adabu Khalwale kwa kujiunga na 'Tangatanga'

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha Ford Kenya kimeanza harakati za kutaka kumwadhibu aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale kwa kujihusisha na kundi la ‘Tangatanga’.

Chama hicho ambacho kinaongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kimemwalika Dkt Khalwale kufika mbele ya kamati ya nidhamu kabla kuamua ikiwa watamtimua chamani au la.

Dkt Khalwale ambaye ni naibu kiongozi wa Ford Kenya, ni mmoja wa wanasiasa wa kundi la ‘Tangatanga’ linalounga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Bw Wetang’ula ambaye awali alikuwa ametangaza azma yake ya kuunga mkono Dkt Ruto alibadili msimamo na akawa mmoja wa wakosoaji wakuu wa naibu wa rais.

Kamati ya nidhamu ya chama cha Ford Kenya ilimwandikia barua Bw Khalwale Machi 26, mwaka huu ikimtaka kujibu malalamishi dhidi yake. Dkt Khalwale hata hivyo alikataa kujibu barua hiyo.

“Inasikitisha kwamba kufikia sasa umekataa kujibu madai dhidi yako. Kwa sababu wewe ni kiongozi wa ngazi ya juu, tunakuongezea muda na tunakualika kufika mbele ya kamati Mei 23, 2019 saa 3.30 asubuhi,” akasema mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya Ford Kenya, Bw Ferdinand Wanyonyi, kupitia barua iliyoandikwa Mei 13, mwaka huu.

“Uko huru kuja ukiwa umeandamana na wakili wako. Kikao hicho kitafanyika katika makao makuu ya Ford Kenya jijini Nairobi,” akasema Bw Wanyonyi.

Iwapo kamati hiyo itampata na hatia Dkt Khalwale huenda akatimuliwa chamani, kuondolewa kutoka wadhifa wake wa naibu kiongozi wa chama, kukaripiwa na kutozwa faini.

Kamati hiyo pia itapendekeza adhabu iwapo Dkt Khalwale atafeli kujibu barua hiyo kufikia Jumanne wiki ijayo.

“Ikiwa utakosa kujibu barua hii kufikia Mei 21, 2019, kamati itachukulia kwamba umepuuza na itakuwa huru kuzingatia uzito wa madai dhidi yako na kupendekeza adhabu,” akasema Bw Wanyonyi.