KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) Rigathi Gachagua anadai analenga kuunganisha viongozi wa upinzani chini ya mgombeaji mmoja wa urais katika uchaguzi wa 2027, lakini matamshi yake makali dhidi ya washirika wake yameibua wasiwasi.
Bw Gachagua anaendelea kuwakosoa baadhi ya vinara wa upinzani akiwalaumu kwa kutofanya bidii kujenga umaarufu, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayekabidhiwa urais bila kuungwa mkono na wapigakura.
Katika mkutano wake na viongozi nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, Jumanne, kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) alimshambulia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i miongoni mwa wanaomkosoa, akisema baadhi ya washirika wake hawataki kuzungumzia idadi ya kura wanazoweza kuweka mezani
Gachagua alimpiga vijembe Muturi, ambaye anatoka eneo la Mbeere, akisema alishindwa hata kuvutia wapigakura katika kituo chake cha kupiga kura wakati wa uchaguzi mdogo wa MCA.
“Unasema unataka kutusaidia kumuondoa Kasongo, lakini katika uchaguzi wa MCA kituoni kwako uliweza kupata watu 35 pekee, huku Kasongo akipata 238. Unataka kumfundisha Riggy G nini?” alisema.
Aliongeza kuwa hatakubali kufanya kampeni na kuvutia kura ili kuzikabidhi kwa viongozi wengine bila wao kujituma.
“Sitasaka kura nikuletee wewe na mke wako,” alisema, akiwataka wenzake kutoka kwenye hoteli na kuanza kuwashawishi wananchi.
Gachagua pia alifichua kuwa amekuwa akigawa idadi ya kura kwa washirika wake, akisema alimwambia Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alenge kura milioni tano, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka milioni tatu na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa milioni moja.
Kauli hizo zimezua mjadala kuhusu nafasi ya viongozi wengine katika mazungumzo ya kuunda muungano wa upinzani, hasa baada ya Muturi kumshutumu Gachagua kwa kutumia vitisho badala ya kujenga ushirikiano wenye kuheshimiana.
Matiang’i naye amekosoa pendekezo la Gachagua la kuunganisha maeneo ya Mlima Kenya, Ukambani na Magharibi, akisema siasa zinazotegemea idadi ya watu wa maeneo fulani zinaweza kuvunja umoja wa upinzani na kuua ndoto ya muungano dhidi ya Rais Ruto.
Alionya kuhusu kile alichokitaja kama kiburi cha walio wengi kinachoweza kuwatenga viongozi wengine na kufanya mazungumzo ya kupata mgombeaji mmoja kuwa magumu.
Hata hivyo, Gachagua amesisitiza kuwa hana kiburi, bali anasema ukweli kuhusu siasa za uchaguzi.
“Ninapowaambia tuamke tufanye kazi, wanasema ninawanyanyasa. Mimi si mwenye kiburi, nasema ukweli,” alisema.
Katika jitihada za kuimarisha muungano huo, jana Gachagua alikutana na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu nyumbani kwake Wamunyoro. Ngilu alihusika katika kuunda muungano wa NARC uliomuingiza madarakani marehemu Mwai Kibaki mwaka 2002 na kumaliza utawala wa KANU.
Gachagua alisema alijifunza kutoka kwa Ngilu kuhusu mikakati iliyotumiwa kuunganisha vyama vya upinzani na kuhakikisha vinaunga mkono mgombeaji mmoja.
Haya yanajiri baada ya Gachagua kukutana na Kalonzo na Sifuna katika mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kisiasa. Ameashiria kuwa muungano unaojengwa unaweza kujumuisha viongozi hao pamoja na Eugene Wamalwa.
Hata hivyo, hii inaweza kuchukuliwa kwa ishara ya kutokuwa na nia njema na vinara wengine akiwemo Martha Karua, Ndindi Nyoro na Muturi ambao wamekuwa wakihubiri haja ya upinzani kuunga ili kuwa rahisi kumshinda Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, kauli za Gachagua ni hatari kwa upinzani chini ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Anashangaa kwa nini naibu rais huyo wa zamani anatoa kauli tofauti na msimamo wake wa awali kwamba upinzani unaweza kushinda tu iwapo utaungana na kuteua mmoja wao kuwa mgombea urais wa pamoja.
“Kwa maoni yangu, Gachagua anajenga akibomoa. Ukifuatilia kabla ya Sifuna kupata umaarufu, hakuwa akimchangamkia. Sasa kwa vile amevuna, anamleta karibu huku akiwabeza baadhi ya vinara aliokuwa akitangamana nao awali,” asema Dkt Gichuki na kuongeza hii ni hatari.
“Kwa sasa, upinzani unapaswa kuwa ukihubiri umoja na kutoka mwelekeo kwa wafuasi wao lakini inaonekana Gachagua hayuko tayari kwa hili. Kwa lugha ya mtaa, anachafua bahari wakati ambao yeye na wenzake wanafaa kuwa wakijiandaa kuvua,” akasema.
Gachagua anasisitiza kuwa tofauti za ndani hazitazuia upinzani kusimamisha mgombeaji mmoja dhidi ya Rais William Ruto mwaka 2027.