Gavana Kamotho motoni kwa kutaka kumrithi Uhuru
NDUNG’U GACHANE, DPPS Na CHARLES WASONGA
GAVANA Anne Mumbi Kamotho wa Kirinyaga amejipata motoni kwa kuchukua kazi ya Rais Uhuru Kenyatta ya kutangaza msimamo wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya.
Wakosoaji wake wanasema Bi Kamotho amejifanya msemaji wa eneo hilo, wajibu ambao unatambuliwa kuwa wake Rais Kenyatta.
Naibu kiranja wa wengi katika Seneti, Irungu Kang’ata alisema matamshi ya gavana huyo kuwa eneo la Mlima Kenya liko tayari kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022 ni yake binafsi.
Bw Kang’ata, ambaye pia ni Seneta wa Murang’a, alisema eneo hilo lina kiongozi mmoja pekee ambaye ni Rais Kenyatta, ambaye ndiye atawashauri viongozi wa kisiasa kuhusu yule wanayepasa kuunga mkono kwa wadhifa wa urais.
Alisema Bi Kamotho, au kiongozi yeyote yule hapaswi kujifanya kuzungumza kwa niaba ya eneo hilo, akisema matamshi kama hayo ni ya kibinafsi na hayawakilishi msimamo wa eneo zima la Mlima Kenya.
“Maoni yaliyowasilisha na gavana wa Kirinyaga ni yake kama mtu binafsi. Wengine wetu kutoka eneo hili tunasubiri kupata mwelekeo na ushauri kutoka kwa Rais Kenyatta. Kufikia sasa hajatuonyeshwa yule ambaye tunayepaswa kuunga mkono,” akasema Bw Kang’ata.
Wiki jana, Bi Kamotho alinukuliwa akisema kuwa eneo hilo liko tayari kubuni muungano wa kisiasa na Bw Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.
Gavana huyo pia alisema kuwa yuko tayari kuunganisha eneo hilo kisiasa na kuwa msemaji wake.
Kwingineko, baadhi ya wabunge wa chama cha Jubilee kutoka Mlima Kenya wamemshambulia Bw Odinga wakisema anadanganya kuwa hafanyi siasa, huku akiendeleza mikakati ya kujitayarisha kugombea urais 2022.
Wabunge hao walioandamana na Dkt Ruto katika Kaunti ya Meru jana, walisema Jubilee pia inapasa kuanza kujiandaa kwa ajili ya 2022 kama ODM inavyofanya.
Viongozi hao walikuwa ni Seneta Mithika Linturi (Meru), wabunge Mugambi Rindiki (Buuri), Halima Mucheke (kuteuliwa), Charity Kathambi (Njoro), Rigathi Gachagua (Mathira), Catherine Waruguru (Laikipia) na Jayne Kihara (Naivasha).
Wengine walikuwa John Muchiri (Manyatta), John Paul Mwirigi (Igembe Kusini) na Gichunge Kabeabea (Tigania Mashariki).
Bw Linturi alisema wakati umefika kwa Jubilee kufanya uchaguzi wake wa kitaifa ili kuimarisha maandalizi yake ya uchaguzi wa 2022.
Naye Bi Waruguru alisema handisheki inatumiwa vibaya kusaidia Bw Odinga kisiasa: “Tulimkaribisha Bw Odinga nyumbani kwetu kwa ajili ya kuunganisha Wakenya. Lakini sasa ni wazi ilikuwa mbinu ya kumsaidia kuchukua madaraka 2022.”
Dkt Ruto alisema haogopi kupambana na Bw Odinga kwenye uchaguzi wa urais 2022.
Ingawa alikariri kwamba kwa sasa hana haja kuzungumzia masuala kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2022, Dkt Ruto alimtaka Bw Odinga kwanza atangaze wazi kuwa atakubali uamuzi wa Wakenya endapo atashindwa tena uchaguzini.
“Sina shida yoyote kushindana na Bw Odinga 2022, lakini kwanza ahakikishie Wakenya kwamba endapo atashindwa, atakuwa muungwana na kukubali uamuzi wa Wakenya,” akasema alipozuru Kaunti ya Meru.
Matamshi yake yalitokea siku moja baada ya kuripotiwa kwamba Bw Odinga alitangaza nia ya kuwania urais ifikapo 2022.
Lakini Bw Odinga jana alipuuzilia mbali ripoti hizo na kusema kile anachokipa kipaumbele wakati huu ni mchakato wa kupalilia umoja nchini kupitia muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari na msemaji wake Dennis Onyango, mwanasiasa huyo alisema wito aliotoa kwa wafuasi wa ODM Jumamosi ni kwamba wajiandae kwa uchaguzi wa mashinani wala si uchaguzi wa urais.
Bw Odinga alisema wakati huu ambapo imesalia miaka mitatu kabla ya uchaguzi mkuu ujao, wajibu wake ni kuangazia masuala muhimu yanayowakumba Wakenya kama vile kuzorota kwa uchumi, kukithiri kwa ufisadi, changamoto zinazokabili serikali za kaunti na mageuzi katika sekta ya elimu.