Habari

Gesi yakosekana Lamu

March 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

SHUGHULI ya kuchimba gesi ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda wa mwaka mmoja uliopita katika kisiwa cha Pate, Kaunti ya Lamu hatimaye imekamilika, huku gesi ikikosekana.

Shughuli hiyo iliyong’oa nanga rasmi Aprili. 2018 imekuwa ikitekelezwa na kampuni ya Zarara Oil and Gas Limited.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali Jumatatu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Zarara hapa nchini, Peter Nduru, alisema jumla ya mita 4,307 zilichimbwa kwenda chini katika kisiwa cha Pate-2 lakini hadhi ya gesi iliyokuwa ikitafutwa ikakosekana.

Bw Nduru alisema shughuli ya kutafuta gesi hiyo ambayo ilifaa kukamilika tangu Oktoba 2018 ilichukua muda mrefu kutokana na changamoto za mawe magumu ambayo yalikuwa yakivunjwa wakati wa shughuli ya uchimbaji na utafutaji wa gesi hiyo ilipokuwa ikitekelezwa.

Pia kiwango cha juu cha presha ambayo ilipatikana eneo husika ni kiini cha shughuli ya kuchimba na kusaka gesi hiyo kuchukua muda mrefu kinyume na ilivyopangwa awali.

“Tumekamilisha kuchimba kisima cha Pate 2 ambapo gesi iliyoko haiwezi kufikia hadhi ya kibiashara ambayuo tulikuwa tukitafuta. Hii inamaanisha kisima cha Pate 2 kitaachwa hivyo bila ya shughuli yoyote. Aidha tumetambua kuwepo kwa madini ya petroli kwenye eneo linalokaribiana na Kipini. Zarara itaangazia kutafuta madini hayo katika mpangilio ujao,” akasema Bw Nduru.

Baadhi ya vifaa vya kutekelezea shughuli ya kuchimba gesi vilivyokuwa vimefikishwa eneo la Pate, Kaunti ya Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Shughuli ya kuchimba madini hayo ilijiri miaka 48 baadaye kufuatia majaribio yaliyotekelezwa na kampuni ya Shell-BP mnamo 1971, ambapo kisima cha kwanza cha Pate 1 kilichimbwa na madini ya gesi na mafuta kugunduliwa.

Aidha kisima hicho ilibidi kiachwe baadaye baada ya mafuta na gesi iliyopatikana kukosa kuafikia kiwango cha kibiashara.

Tangu 2013 aidha, kampuni ya Zarara imekuwa ikitekeleza utafiti na ukaguzi wa madini hayo kabla ya kuafikia hatua ya kuchimba kisima cha Pate 2 mnamo Aprili mwaka jana.

Mradi wa kuchimba gesi kwenye kisiwa cha Pate ulikuwa miongoni mwa miradi mingine mikuu ambayo inatarajiwa kubadili hali ya uchumi, biashara na viwanda kote Lamu.

Miradi mingine ni pamoja na ule wa Sh 2.5 trilioni wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) eneo la Kililana, mradi unaotarajiwa kuanza wa Sh 200 bilioni wa nishati ya makaa ya mawe eneo la Kwasasi, tarafa ya Hindi na ule wa Sh 21 bilioni wa nishati ya upepo eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni.