Gunia la mahindi kilo 90 linunuliwe kwa Sh2,500, aagiza Rais
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi ameamuru Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuanza kununua magunia 2 milioni ya mahindi kutoka kwa wakulima kote nchini kwa bei ya Sh2,500 kwa gunia la kilo 90.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari Alhamisi jioni Ikulu ya Rais ilisema NCPB inafaa kufungua mabohari yake kote nchini ili kupokea mahindi kutoka kwa wananchi.
“Nimemwagiza Waziri wa Kilimo kutoa idhini kwa Bodi ya Kitaifa na Nafaka na Mazao kupitia Shirika la Uhifadhi wa Chakula, kwa ushirikiano na serikali husika za kaunti, kufungua vituo vya ununuzi na maghala ili kupokea mahindi kutoka kwa wakulima kote nchini. Shirika la Uhifadhi wa Chakula (SFR) imepewa idhini ya kununua magunia milioni mbili ya mahindi kwa Sh2,500 kwa gunia moja la kilo 90,” akasema Rais Kenyatta.
Bei hiyo inaashiria kuwa serikali imeongeza bei ya zao hilo kwa Sh200 kutoka bei ya Sh2,300 iliyoweka mwishoni mwa mwaka 2018 na ambayo wakulima na wanasiasa kutoka eneo la North Rift kunakokuzwa mahindi kwa wingi walikataa.
Wabunge Silas Tiren (Moiben), Alfred Keter (Nandi Hills) na Joshua Kutuny (Cherangany) waliowaongoza wakulima kuitaka serikali iongeze bei hiyo hadi kufikia Sh3,600,wakisema watapata hasara kubwa ikiwa watauza mahindi yao kwa Sh2,300.
Faida
“Bei ya Sh2,300 itawafanya wakulima kupata hasara kubwa hali ambayo itawavunja moyo na kupelekea baadhi yao kutopanda mahindi msimu ujao. Tungeiomba kuipandisha bei hiyo hadi Sh3,600 ili wakulima waweze kupata faida kwa sababu gharama ya uzalishaji ipanda kutokana ongezeko la bei ya mafuta na fatalaiza na pembejeo nyinginezo,” akasema Bw Tiren.
Lakini Alhamisi Rais alisema serikali iliweka bei hiyo (ya Sh2,500) kutokana na mavuno mazuri ambayo wakulima walipata katika msimu wa 2018 baada ya serikali kupiga jeki kilimo cha mahindi kwa njia mbalimbali.
“Kufuatia hatua ambazo serikali ilichukua kuimarisha kilimo cha mahindi pamoja na hali nzuri ya anga, tulipata mavuno mazuri ya kima cha magunia 46 milioni. Vile vile, kuna takriban magunia 2.5 milioni katika maghala kutokana na mavuna ya mwaka wa 2017. Hizi ni miongoni mwa sababu ambazo zimeifanya serikali kuweka bei ya Sh2,500,” Rais Kenyatta akasema.
“Kwa hivi serikali itatoa magunia 1.7 milioni ya mahindi ya uzani wa kilo 90 na kuyauza kwa Sh1,600 kwa kila gunia na magunia mengine 300,000 ya mahindi ya kutumia kutengeneza lishe ya mifugo kwa Sh1,400 kwa kila gunia,” akaongeza.
Kulingana na Rais Kenyatta, kuna mahindi tosha katika nchini ambayo yanauzwa kwa kati ya Sh1,700 na Sh1,800 kwa gunia la kilo 90.
Kiongozi wa taifa pia aliyataka mashiriki husika kuhakikisha yanakamilisha shughuli ya kuthibitisha wakulima halisi watakaowasilisha mahindi yao kwa NCPB ili walipwe haraka.
Rais Kenyatta alikariri kuwa serikali yake imejitolea kupiga jeki wakulima kama njia ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini. “Kwa njia hii nimeiagiza wizara ya kilimo kuharakisha utekelezaji wa mikakati iliyoafikiwa chini ya mwavuli wa Ajenda Nne Kuu inayohusiana na uzalishaji wa chakula toshelezi.