Bunge la Mwananchi: Kenya Kwanza yajihusisha na kampeni za mapema badala ya kuwajibika
RAIS wa Bunge la Mwananchi, Francis Awino, ametoa wito kwa vijana na wananchi kwa jumla kudai uwajibikaji, uwazi, na uongozi bora kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza, akisema kuwa taifa linapoteza mwelekeo kwa sababu ya uongozi mbaya.
Akizungumza na vijana jijini Nairobi Ijumaa (Aprili 4, 2025), Bw Awino alikosoa mienendo ya kisiasa ya viongozi wa sasa, akisema kuwa wanajihusisha na kampeni za mapema badala ya kushughulikia matatizo yanayoikumba nchi, kama vile ukosefu wa ajira na gharama ya juu ya maisha.
“Katiba ya Kenya chini ya Kifungu cha 43 kinasema kuwa kila Mkenya ana haki ya kupata makazi bora, chakula, na huduma za afya. Lakini badala ya kuyatekeleza haya, serikali imejikita kwenye kampeni za mapema,” alisema Bw Awino.
Bw Awino pia alieleza wasiwasi wake kuhusu hatua za Rais William Ruto, akidai kuwa amekuwa akijitangaza kama msemaji wa kisiasa wa maeneo mbalimbali kama vile Nyanza na eneo la Mlima Kenya badala ya kuunganisha taifa.
“Ni wakati wa kuangazia matatizo halisi yanayowakumba wananchi, sio maneno matupu ya kisiasa,” aliongeza.
Aidha, alikemea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akidai imeshindwa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, na akatoa wito wa marekebisho ili kulinda demokrasia nchini.
Rais huyo wa Bunge la Mwananchi aliwahimiza vijana kushikilia msimamo thabiti na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mageuzi ya kijamii na kiuchumi, akisema huu ndio wakati wa “ukombozi wa tatu” wa Kenya.
“Wale wanaojihusisha na siasa kwa manufaa ya kibinafsi waendelee, lakini sisi vijana lazima tuwe macho kuiboresha na kuikomboa nchi yetu,” alisisitiza.
Kando na hayo, alitoa wito kwa wananchi wote kushirikirikiana ili kuiwajibisha serikali, akisema kuwa taifa bora linahitaji ushirikiano.
“Wakati wa mabadiliko umefika. Kenya iliyo na haki na usawa inawezekana ikiwa kila mmoja atatekeleza jukumu lake,” alisema.